Header Ads Widget

BAVICHA Waunga Mkono Oparesheni UKUTA........Wasema Maandalizi Yote Yamekamilika, Wasisitiza Kutorudi Nyuma Septemba Mosi


BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limetangaza kuunga mkono operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta (Ukuta) iliyotangazwa hivi karibuni na Kamati Kuu ya chama hicho.

Aidha, Bavicha wamemjibu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwamba hana mamlaka ya kuzuia operesheni hiyo kwa kuwa wanaifanya kisheria na yeye siyo msajili wa vyama vya siasa.

Makonda aliagiza Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya Ukuta, Ijumaa wakati akizungumza na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika kambi ya Ukonga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi, alisema maandalizi ya kuunga mkono operesheni hiyo yamekamilika kwa nchi nzima.

“Kauli ya Mkuu wa Mkoa (wa Dar es Salaam) ya kusema kwamba polisi wahakikishe Ukuta haujengeki, haitekelezeki kwa sababu yeye hana mamlaka ya kufanya hivyo na wala si msajili wa vyama vya siasa hadi atoe kauli hiyo,” alisema Katambi.

“Zipo kesi nyingi zinazoonyesha wakuu wa mikoa kufanya kazi ambazo haziwahusu, hivyo kauli yake tutaipima kisheria,” alisema na kuongeza:

“Yeye akitaka aendelee kusema chochote akijisikia, lakini sisi tunamwambia kwamba mikutano yetu iko pale pale na tutaifanya nchi nzima.”

Katika mazungumzo yake na FFU, Makonda alisema askari wanafahamu sheria, hivyo wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha juu ya jambo hilo.

Aidha, aliwataka polisi hao kutosubiri maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais John Magufuli ameshaagiza kutofanyika kwa maandamano ya Ukuta yaliyopangwa kuwa Septemba mosi.

Makonda aliliagiza jeshi hilo kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwapo kitu kinaitwa Ukuta ili wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.

Lakini Mwenyekiti wa Bavicha jana alisema: “Tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ajiandae kutuma jeshi lake kulinda mikutano yetu.”

Kuhusu onyo la Rais Magufuli aliloitoa akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Singida kwamba Chadema isimjaribu kwa Ukuta, Katambi alisema chama hicho hakimjaribu.

Alisema Chadema itafanya maandamano nchi nzima kwa sababu kwa njia hiyo wanamsaidia kutoa mawazo yao kama vyama vya siasa kwa ajili ya kumsaidia kuendesha shughuli zake vizuri zaidi.

“Hatuna shida ya kumjaribu Rais, na wala si kwamba tunamchukia, na wala hatuna sababu ya kupinga uwapo wake, na hata ukiulizwa sasa kwamba Rais wako ni nani, lazima useme ni John Magufuli,” alisema Katambi.

“Tunapotoa dosari na kasoro tunamsaidia kuendesha nchi yake na watu walio chini yake.”

“Sisi kama vyama vya siasa tuna haki, tunajua yeye ndiye Rais, kama sisi hatukuweza kupata nafasi ya hiyo, haimaanishi kwamba ni vita, isipokuwa kupitia vyama vyetu, tuna sehemu ya kutoa mawazo yetu katika kuifanikishia serikali yake kuongoza vema pamoja na watu wake wa chini tena kwa mujibu wa sheria na inamsaidia yeye kuwa bora zaidi.
“Kwa hiyo kauli ya Rais sisi hatuna tatizo nayo.”

Katambi alisema taratibu zote za kisheria katika kutekeleza mikutano hiyo zitafuatwa.

Kamati Kuu ya chama hicho ilisema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini.

Post a Comment

0 Comments