Header Ads Widget

Kiwanja Cha Ndege Dodoma Kukamilika Mwishoni Mwa Agosti


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa vitendo wakati alipokagua maendeleo ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Dodoma.

Imeelezwa kuwa upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege  cha Dodoma utakamilika mwishoni mwa mwezi Agosti ili kuruhusu ndege za abiria sabini mpaka tisini kuweza kutua na kuruka na hivyo kurahisisha usafiri wa anga kwa ukanda wa kati.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa baada ya  kutembelea  kiwanjani hapo kukagua hatua ya mwisho ya ujenzi iliyofikiwa ambapo amesema kasi ya Mkandarasi Chicco anayetekeleza kazi hiyo inaridhisha katika kuhakikisha kiwanja hicho kinakamilika kwa muda na kwa viwango vilivyokubalika.

Amesema mpaka sasa ni asilimia themanini ya kazi iliyotekelezwa kwa siku arobaini na tano tangia kuanza ukarabati hivyo kasi iliyotumika kwenye kiwanja hiki itatumika kwenye ujenzi wa viwanja vingine nchini.

"Tunaamini kabisa kwa kasi ya mkandarasi na msimamizi mtakamilisha ujenzi huu haraka na viwango tulivyokubaliana katika mkataba ili ndege kubwa zianze kutua na kuruka" amesema Prof. Mbarawa.

Naye Msimamizi wa ujenzi wa kiwanja hicho kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Eng. Mhandisi Mbila Mdemu amesema kazi ya ukarabati na upanuzi inaendelea kufanywa usiku na mchana kwa kuzingatia ubora na viwango na kukamilika kwa wakati

"Tulipewa kazi hii na tunaahidi kuwa  itakamilika kama tulivyoelekezwa ili kuwapa wananchi wanaozunguka mikoa ya Dodoma na jirani fursa ya kutumia usafiri wa Anga", amesema Eng. Mdemu.

Ameongeza kuwa kazi zinazokamilishwa sasa ni kumalizia sehemu ya maegesho ya ndege na tabaka la mwisho kwenye barabara  ya kuruka na kutua ndege.

Mradi wa upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha  ndege cha Dodoma umegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa zaidi ya shilingi bilioni 11.8 na kukamilika kwake kutaongeza idadi ya safari za ndege zitakazosafirisha abiria wa mikoa ya kanda ya kati.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipokea taarifa ya maendeleo ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Dodoma kutoka kwa Eng. Guo Zhingjian wa kampuni ya Chicco inayojenga kiwanja hicho, Mkoani Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa kutoka Eng. Guo Zhingjian wa kampuni ya Chicco inayojenga kiwanja hicho Mkoani Dodoma.

Post a Comment

0 Comments