MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ameitisha Baraza la Vyama vya Siasa ili kunusuru mvutano uliojitokeza kati ya Jeshi la Polisi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Jaji Mtungi amevitaka vyama vya siasa vilivyotangaza kufanya maandamano na mikutano isiyo na tija nchi nzima kuacha, badala yake warudi kwenye meza ya mazungumzo ili kuondoa tofauti zinazojitokeza.

Kauli ya Jaji Mutungi imekuja baada ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) nao kutangaza maandamano ya amani kwa ajili ya kupongeza utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli, huku Chadema kikiitisha maandamano na mikutano isiyo na kikomo nchi nzima, ambayo imepewa jina la Operesheni Ukuta.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema kufanyika kwa maandamano na mikutano hiyo, hakuwezi kuondoa changamoto za kisiasa zilizopo, hivyo basi wanapaswa kukaa kwenye meza moja kwa ajili ya kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.

“Ninawaomba wale wote wenye lengo la kuitisha maandamano na mikutano ya kisiasa kuacha kwa sababu haiwezi kusaidia kuondoa changamoto zilizopo, bali tunapaswa kukaa kwenye meza moja ya mazungumzo ili tuweze kujadili tofauti hizo na kuzipatia majibu,”alisema Jaji Mutungi.

Aliongeza kuwa licha ya kuwapo kwa jitihada za viongozi mbalimbali kujadili suala hilo, lakini vyama hivyo vimeonekana bado vikiendelea na misimamo yao ya kuitisha mikutano na maandamano yasiyo na kikomo, jambo ambao linaweza kuleta hofu kwa wananchi.

Jaji Mutungi alisema katika kipindi hiki ambacho wananchi wametulia, hakuna haja ya kuwatia hofu au wasiwasi ili ionekane kuwa nchi ina ombwe kubwa la uongozi, jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma juhudi za kuleta maendeleo.

Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuheshimu utawala bora na kuacha kujadili mambo ambayo yanaweza kuvuruga amani, badala yake wanapaswa kuangalia mustakabali wa taifa kwa kufanya kazi na kuleta maendeleo.

“Wananchi wanapaswa kuondoa hofu kuhusiana na migongano ya kisiasa inayojitokeza, kwa sababu hakuna ombwe la uongozi, badala yake wanapaswa kufanya kazi kwa masilahi ya taifa ili waweze kuleta maendeleo,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, ameamua kuitisha mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa ambalo linashirikisha vyama 22, vikiwamo CCM na Chadema wajadili mambo mbalimbali ikiwamo migongano ya kisiasa, ili waweze kuendesha shughuli zao kistaarabu.

Alisema mkutano huo utafanyika Agosti 29 na 30 mwaka huu ukishirikisha wadau mbalimbali.

Jaji Mutungi alisema kutokana na hali hiyo, Agosti 26 kutakuwa na kikao cha kuratibu mkutano huo ambao anaamini ni muhimu kwa ajili ya kuleta maridhiano baada ya tofauti za kisiasa zilizojitokeza.

“Baraza hili ni forum muhimu ya upatikanaji wa maridhiano ya kisiasa kama kuna tofauti zilizojitokeza, kuliko kuitisha mikutano na maandamano yasiyo na tija ambayo yanaweza kusababisha wananchi kupata hofu,” alisema.

Alisema hakuna jambo lenye ugumu katika suala hilo, kwa sababu migongano iliyopo inajadilika ikiwa ni pamoja na kupitia baadhi ya vifungu vya kisheria kwa ajili ya kufatuta mwafaka.

Akizungumzia suala la Chama cha Wananchi (CUF), Jaji Mutungi alisema  migongano iliyopo kwenye chama hicho anaijua, lakini kwa sasa hawezi kuzungumzia lolote kwa sababu mkutano ujao utashirikisha vyama vyote kikiwamo CUF.

“Mimi ni mlezi wa vyama vya siasa… CUF ni miongoni mwa watoto wangu, najua udhaifu wa vyama vyote kikiwamo CUF hadi ubora wao, hata migongano iliyojitokeza ndani ya chama hicho naijua, lakini kwa sasa nashindwa kuongea lolote kwa sababu tuna mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa ambalo litajadili mambo mbalimbali, ikiwamo suala la mgogoro wa CUF,” alisema Jaji Mutungi.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wanachama wa chama hicho kuondoa hofu kwa sababu suala hilo litapatiwa ufumbuzi kwa kuondoa tofauti zilizopo.

Jaji Mutungi aliyesema hayo huku wafuasi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, wakidai kwenda katika ofisi yake kumweleza mambo mbalimbali, ikiwamo ya ukiukwaji wa taratibu za kisheria na kumwondoa kiongozi huyo kwenye nafasi yake uliofanywa na wafuasi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika hatua nyingine, Chadema kimesema kimesikia wito wa Jaji Mutungi wa kuitisha mazungumzo ambayo iwapo yatatawaliwa na nia njema na dhamira safi ya kuheshimu Katiba ya nchi, yanaweza kuwa na manufaa kwa Watanzania wote.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama  hicho, Tumaini Makene, ilisema hatua hiyo inaweza kuleta manufaa kama Jaji Mutungu hataegemea upande wa Serikali.

“Wakati Msajili wa Vyama akitoa kauli ya kuzuia kile anachokiita ‘kutunishiana misuli’, Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali limeingilia vikao vya ndani vya chama na kuzuia visiendelee. Hiyo yote ni kinyume  na sheria, taratibu na mamlaka yao.

“Mbali na kuzuia vikao vya ndani, Jeshi la Polisi linashikilia watu mbalimbali, wakiwamo wafuasi, mashabiki, wanachama, viongozi wetu  kwa kushiriki vikao hivyo, wakitekeleza wajibu na haki zao za kikatiba na kisheria.

“Wakati tunasubiri meza ya mazungumzo kupitia Baraza la Vyama, tunapenda kusisitiza kuwa Chadema itasimama imara kuhakikisha misingi ya demokrasia na utawala unaozingatia Katiba na sheria unafuatwa,” ilisema taarifa hiyo.