SAED Kubenea Mbunge wa Jimbo la Ubungo jana alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kuhojiwa kabla ya kupewa dhamana kufuatia tuhuma za kuandika makala inayodaiwa kuwa ya uchochezi kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar.

Kubenea ambaye anadaiwa kufanya uchochezi kwa kuandika makala katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 349 la Julai 25-31 yenye kichwa cha habari, ‘Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar?’

Kubenea alifika katika kituo hicho cha Polisi jana  saa saba na robo mchana (13:15) akiwa na Tundu Lissu Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na Frederick Kihwelu wakili mwandamizi wa Chama hicho.

Baaada ya kuhojiwa kwa zaidi ya masaa mawili, saa tisa na robo alasiri (15:45) alitoka na kuondoka huku wandishi wa habari wakishindwa kuzungumza naye baada Jeshi la Polisi kuwazuia waandishi wa habari kuingia katika eneo la kituo hicho.

Akizungumza kwa njia ya simu, Lissu ambaye ndiye mwanasheria wa Kubenea katika sakata hilo alisema kuwa, Kubenea amehojiwa kwa madai ya uchochezi lakini alichokiandika ni hali halisi ya Zanzibar hususani visiwa vya Pemba.

“Kubenea amechiwa kwa dhamana na ameamriwa kurudi tena kituoni hapo tarehe 18 Agosti, mwaka huu,”alisema Lissu.

Katika makala yake inayodaiwa kuwa ni ya kichochezi iliyokuwa na kichwa cha habari, “Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar?” Kubenea alielezea jinsi Jeshi Polisi Visiwani Pemba wavyonadaiwa kuwabambikia kesi wananchi, kuwapiga na kuwatesa kwa madai kuwa wananchi hao wanaipinga serikali.

Kubenea aliandika Makala hiyo baada ya kusafiri kutoka Dar es Salaam Mpaka Zanzibar kufuatilia kile alichokitaja kama mateso, unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi wasio na hatia visiwani humo.

Miongoni mwa vijana na wahanga wa kubambikiwa kesi, kupigwa na kuteswa visiwani Pemba waliotajwa na Kubenea katika makala yake ni ni Hijja Hassani aliyetangazwa kuwa ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani kabla ya Jecha Salim Jecha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi.