Baada ya kufanya uhakiki wa Wanafunzi Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umebaini uwepo wa wanafunzi hewa 2331 katika shule za Sekondari za Mkoa huo.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka wakati alipozungumza na Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata mara baada ya kuwakabidhi Vishikwambi (Tablets) vilivyotolewa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la EQUIP Tanzania kwa ajili ya utunzaji wa Takwimu muhimu za Sekta ya Elimu,.
Mtaka amesema kati ya Halmashauri sita za Mkoa huo, Ni Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi tu ambayo haina wanafunzi hewa wakati Halmashauri ya Wilaya ya Busega ikiwa na wanafunzi hewa 110, Itilima 2137, Maswa 14, Meatu 125 na Halmashauri ya Mji wa Bariadi 439.
Kufuatia kuwepo kwa wanafunzi hewa Mkuu wa Mkoa huo amesema, Serikali Mkoani humo imepanga kufanya mabadiliko ya Wakuu wa Shule za Sekondari katika Mkoa mzima, wakati taratibu za kinidhamu zikiendelea kwa wakuu wa shule waliotoa takwimu za uongo za wanafunzi katika shule zao, wakati kwa upande wa shule za Msingi, mabadiliko yatafanyika baada ya kumaliza mtihani wa darasa la saba.
Mtaka amesema kabla ya uteuzi wa wakuu wa shule na walimu wakuu utafanyika upekuzi (vetting) kwa wale watakaopendekezwa ili kujiridhisha kama wahusika wana sifa na uwezo wa kuendesha shule na kusimamia fedha za Serikali zinazopelekwa shuleni kwa ajili ya kugharama elimu ya bila malipo.
“ Serikali inaendelea kupelekea fedha moja kwa moja katika akaunti za shule, kwa hiyo mkuu wa shule au mwalimu mkuu ni afisa masuuli katika shule yake. Ipo haja kwa sisi kujiridhisha kama Serikali kuwa anayeteuliwa kushika nafasi ya kuongoza shule ana uwezo na sifa ya uadilifu. Sitakuwa tayari kuona katika mkoa huu kuna walimu wakuu wazoefu wa kula fedha za Serikali na wakaendelea kuongoza shule”alisema Mtaka.
Akitoa shukrani kwa Shirika la EQUIP Tanzania, Mkuu wa Mkoa amesema Shirika hilo limekuwa msaada katika kutatua baadhi ya changamoto za Watendaji katika Sekta ya Elimu mkoani Simiyu ikwa ni pamoja na kuwawezesha Waratibu Elimu Kata kwa kuwapa pikipiki na kuwapa fedha za mafuta shilingi 206,000 kwa kila mwezi pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wakuu na walimu wakuu wasaidizi.
Aidha, Mtaka amesema analishukuru shirika hilo kuona umuhimu wa kutoa vishikwambi kwa Walimu wakuu na Waratibu Elimu Kata ambavyo ameelekeza vitumike kutunza takwimu sahihi za kieleimu ikiwemo idadi ya walimu na wanafunzi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amewataka Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata kuvitunza vishikwambi hivyo na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Naye Mkuu wa EQUIP Tanzania Mkoa wa Simiyu, Phoebe Okeyo amesema Vishikwambi hivyo vitawasaidia Viongozi wa Elimu ngazi ya Mkoa, Wilaya na kata kupata taarifa za masuala mbalimbali yanayofanyika shuleni.
“Sasa hivi mtegemee kupata taarifa sahihi katika sekta ya Elimu kwa sababu ya hivi vifaa tulivyovitoa leo, tumeanza kama pilot study kwa Mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara, Tabora, Dodoma,Lindi na Kigoma. Tunatarajia kuongeza mikoa ya Katavi na Singida Januari, 2017” alisema Okeyo.
Jumla ya Vishikwambi(tablets) 637 vimetolewa kwa Walimu wakuu 516 na Waratibu Elimu Kata 121 kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu, ambapo kila kimoja kina thamani ya shilingi 315,000/=.
0 Comments
on