Wasanii wanne wa kundi la vichekesho la Orijino Komedi akiwamo meneja wao wamekamatwa na kuhojiwa na jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kosa la kuwa na sare za polisi. 

Juzi, jeshi hilo lilitoa onyo kwa mtu ama kikundi chochote kuacha kutumia mavazi yanayofanana na sare zinazovaliwa na majeshi ya ulinzi na usalama nchini na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Makosa ya Jinai, sura ya 16 na marejeo yake ya mwaka 2002, kifungu cha 178 (1) na (2) kinachozungumzia makosa dhidi ya sare za majeshi ya ulinzi na usalama, kinabainisha kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama kuvaa mavazi yanayotumiwa au kushabihiana na sare za majeshi hayo bila kibali kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Kaimu Kamanda wa Kanda hiyo, Hezron Gyimbi alisema wasanii hao walikamatwa juzi saa 10 jioni baada ya kusambaa kwa video kwenye mitandao ya kijamii wakiwa wamevalia sare hizo kwenye sherehe ya harusi ya Emmanuel Mgaya maarufu ‘Masanja’. 

Gyimbi aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Lucas Lazaro (Joti), Alex John (McRegan) na Isaya Gidion (Wakuvanga) na Sekioni David (Seki) ambaye ni meneja wao. 

Alisema sare walizokutwa nazo watuhumiwa hao ni za kazi za kawaida za jeshi la polisi hilo ikiwamo kofia, filimbi, shati, suruali, cheo na mkanda. 

“Tunaendelea kuwachunguza zaidi kama wana vitu vingine vya jeshi la polisi na tunataka kujua kuwa sare hizi wamepa- ta kibali kwa nani na uhalali wa kuwa nazo,” alisema Gyimbi. 

Alisema jeshi hilo linaendelea kumtafuta Masanja ili kujibu tuhuma zinazomkabili. Kaimu kamanda huyo alisema watuhumiwa hao walihojiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kuanzia juzi saa 10 jioni hadi jana jioni huku na dhamana zao zilikuwa wazi.