Header Ads Widget

MLO SAHIHI KWA WAGONJWA WA KISUKARI

LEO tutazungumzia mlo sahihi kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari (Diabetes) ambao umeenea nchini, kwani idadi ya walionao inaongezeka kila mwaka, hivyo tahadhari inahitajika. Wataalamu wetu wanauelezea ugonjwa wa kisukari kuwa unatokana na kuvurugika kwa mfumo wa uvunjaji wa kemikali mwilini (Metabolic Disorder) ambao husababisha mwili kushindwa kutumia glukosi (sukari) kikamilifu, hivyo kusababisha mkusanyiko mkubwa wa sukari kwenye damu. Hali hiyo hutokea baada ya kiungo kiitwacho kongosho (Pancreas) kushindwa kutoa homoni aina ya Insulin ambayo ndiyo hudhibiti kiwango cha sukari kinachotakiwa kubaki kwenye damu.


Hali hiyo ya kuvurugika kwa mfumo mzima wa kudhibiti sukari mwilini hutokea baada ya mwili kukosa chakula chenye kirutubisho muhimu katika kuliwezesha kongosho kufanya 
kazi yake ipasavyo, kwa maana hiyo ulaji wako wa chakula hauko sahihi ndiyo maana hali hiyo imetokea. Kwa mujibu wa wataalam wetu, kuna aina mbili za ugonjwa wa kisukari, ambazo ni Type1 na Type2. Type 1 huwapata zaidi watoto au vijana wadogo na hutibika zaidi kwa kutumia
dawa Insulin. Lakini aina ya pili ya kisukari (Type2) ambayo huwapata zaidi vijana kuanzia umri wa miaka 40, watu wanene na wazee, huweza kudhibitiwa kwa kufanya mazoezi na kula mlo uliokamili (Balanced Diet).

MLO WA WAGONJWA WA KISUKARI
Mtu mwenye kisukari ambacho hakijakomaa, anaweza kukidhibiti kwa 
mlo tu bila kutumia dawa yoyote na akaweza kuishi bila matatizo. Lakini kisukari kilichokomaa kinahitaji mlo pamoja na dawa na ili muathirika ajiepushe na madhara makubwa ya ugonjwa huo yanayoweza kumpata ni lazima ahakikishe anafuata masharti ya vyakula. Mtu mwenye ugonjwa wa kisukari anatakiwa kupunguza ulaji wa vyakula vyenye wanga (Carbohydrates), kama vile viazi, mihogo, mikate myeupe (White Bread), n.k. apunguze ulaji wa vyakula vya mafuta na kula vyakula vya proteini kwa kiasi kidogo. Badala yake mgonjwa huyu anapaswa kutumia kwa wingi vyakula vyenye kiasi kikubwa cha kirutubisho kiitwacho ufumwele (Fibre) ambacho hupatikana kwenye vyakula kama vile matunda, nafaka zisizokobolewa (ugali wa dona, ugali wa mtama, mikate myeusi, n.k) na aachane kabisa na kula vyakula vilivyosafishwa (Refined Foods) na kuondolewa virutubisho vyake (mikate myeupe, ugali mweupe, n.k).` Itaendelea wiki ijayo.