Na Ismail Ngayonga - Maelezo.
SERIKALI inakusudia kuwapeleka katika kambi za mafunzo ya Jeshi la Kuujenga Taifa (JKT) watoto wa mitaani wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ili wajifunze stadi za kazi na shughuli za uzalishaji mali.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa mahojiano maalum katika kipindi cha Tunatekeleza kinachoandaliwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na Televisheni ya Taifa (TBC1).
Waziri Ummy alisema hatua hiyo inalenga kuliwezesha kundi hilo la vijana kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali badala ya kuzurura hovyo mitaani sambamba na kujihusisha na tabia na vitendo vinavyokiuka maadili katika jamii.
Alisema tayari watendaji wa Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Waziri Mkuu tayari wamekutana kujadiliana kuhusu suala hilo ili kuangalia namna bora zaidi ya kusadia kundi hilo.
Alifafanua kuwa vituo vingi vya kulelea watoto hao vimekuwa na watoto waliozidi umri wa miaka 18, ambapo kwa mujibu wa sheria hawatakiwi kuwa katika vituo hivyo na kuongeza kuwa ofisi yake itahakikisha zoezi la kuwapeleka katika mafunzo hayo linatekelezeka.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy alipiga marufuku tabia za baadhi ya watu, asasi na vikundi kuanzisha vituo vya kulea watoto yatima pasipo kuwa na usajili kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy alisema tayari ofisi yake imetoa maelekezo kwa Kamishina wa Ustawi wa jamii kufanya tathimini na utafiti wa kina kuhusu vituo vya kulea watoto yatima, ambapo iwapo kutabainika vituo vitakavyokosa sifa hatua za kisheria zitachuliwa kwa wahusika.
Kuhusu chanjo, Waziri Ummy alisema Serikali itaanza kutoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa watoto wenye umri wa miaka 9-13 ili kukabiliana na changamoto ya maradhi hayo nchini.
Waziri Ummy aliwataka wazazi kutoa ushirikiano pindi zoezi hilo litakapoanza kwa kuwa halitakuwa na madhara ya kiafya kwa watoto wao.
Aidha, alisema Serikali imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka kwa ajili ya matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi kwa akina mama ambayo inaambukizwa na virusi vinavyojulikana kwa jina la Human Papiloma Virus (HPV).
“Tumeamua kuteua kundi la watoto wa lika huo kwani wengi wao katika umri huo wanakuwa bado hawajaanza kujihusisha na vitendo vya mapenzi” alisema Waziri Ummy.
Alisema katika bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali imepanga kuipatia taasisi ya saratani ya ocean road kiasi cha Tsh. Bilioni 3 kwa ajili ya ununuzi wa madawa, ikilinganishwa na kiasi cha Tsh. Milioni 600 zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2015/16.
Akizungumzia changamoto iliyojitokeza hivi karibuni ya ukosefu wa chanjo katika vituo vya huduma ya hivi nchini, Waziri Ummy alisema suala hilo litakuwa historia hivi karibuni kwani tayari Serikali imeagiza kutoka nje ya nchi baadhi ya chanjo hizo.
0 Comments
on