Wapangaji katika jengo la ghorofa tano la NSSF lililopo mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera wamezikimbia ofisi zao kwa hofu ya usalama kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni.

Baadhi ya ofisi zilizopo katika jengo hilo ni Tanesco Mkoa wa Kagera, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na NSSF yenyewe ambayo watumishi wake wamelazimika kutoa huduma wakiwa kwenye uzio.

Meneja wa Sumatra Mkoa wa Kagera, Patrick Machia amesema alikuwa anaendelea na kazi nje ya ofisi na kushauri atafutwe msaidizi wake kwa ajili ya kutoa ufafanuzi.

Nje ya jengo hilo wameonekana watumishi wa Tanesco wakiendelea kutoa huduma kwa wateja wakiwa na meza na viti vyao na mlinzi aliyekuwapo katika mlango wa kuingilia kwenye jengo hilo amesema hapakuwa na mfanyakazi yeyote ndani na huduma zote zilikuwa zinatolewa nje.

Kaimu Meneja wa NSSF Mkoa wa Kagera, Siraji Kisaka amesema timu ya wataalamu imeshafika kufanya tathmini ya jengo na baada ya hapo itatoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na jengo hilo.

“Nakushauri upate majibu sahihi kesho, tayari imetumwa timu ya wataalamu kufanya tathmini na kazi imeanza. Baada ya timu kumaliza kazi tutakuwa na majibu sahihi,” amesema Kisaka