Habari kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mji Mkuu Kinshasa zinasema kumetokea mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama ambapo watu 17 wamefariki dunia, miongoni mwao raia 14 na polisi watatu.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa mapigano hayo yametokea majira ya jana asubuhi kabla ya maandamano ya kutaka Rais Joseph Kabila ajiuzulu, maandamano ambayo yalifutwa na serikali.
 
Kufuatia ripoti hizo za vifo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameelezea wasiwasi wake juu ya ghasia hizo mjini Kinshasa na kwenye maeneo mengine ya DR Congo akilaani ghasia zilizotokea.

Ban ametoa wito kwa viongozi wote wa kisiasa na wafuasi wao kujizuia na ghasia zinazoweza kusababisha hali kuwa mbaya zaidi.