Viongozi
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamekimbilia mahakamani kupinga
matokeo ya uchaguzi wa umeya na naibu meya wa Manispaa ya Kinondoni
katika Jiji la Dar es Salaam uliompa ushindi Diwani wa Msasani, Benjamin
Sitta wa CCM kuwa Meya.
Ukawa
kupitia kwa Wakili wao, John Mallya wamewasilisha kesi hiyo jana katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupinga matokeo ya
uchaguzi uliofanyika Oktoba 23 mwaka huu, kwa kuwa ulikuwa batili na
ulikiuka taratibu za kisheria.
Mallya
alisema kesi hiyo ambayo walalamikaji ni aliyekuwa Naibu Meya wa
Manispaa hiyo, Jumanne Mbunju na aliyekuwa mgombea wa umeya, Diwani wa
Kata ya Kinondoni, Mustafa Muro, imepokelewa lakini haijafunguliwa.
Mbali
na Sitta, walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Meya, Manyama
Mangaru, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni,
Aron Kagurumjuli na Ofisa Tawala wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza
baada ya kesi hiyo kupokelewa, Wakili Mallya alisema wamefungua kesi
hiyo kupinga kile wanachoita uchaguzi ambao CCM walikaa wenyewe na
kupigiana kura.
Alisema: “Katika
kesi hiyo tunaiomba Mahakama itengue uamuzi uliomchagua meya huyo,
iamuru manispaa iitishe uchaguzi wa umeya mara moja pia imuamuru
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa na wasimamizi wa uchaguzi wafuate
taratibu za kisheria.”
Katibu
wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo alisema wamefika
mahakamani kutafuta haki kwa sababu wanaamini wamenyang’anywa haki yao.
Alisema
kilichosababisha uchaguzi wa Ubungo kuahirishwa ni kukiukwa kwa
taratibu hivyo Mkurugenzi na Ofisa Tawala wa Ubungo walipoona taratibu
zimekiukwa Kinondoni, waliamua kuahirisha uchaguzi.
“Kilichofanyika
siku ile ilikuwa ni kuchagua Mwenyekiti wa CCM, lakini siyo uchaguzi wa
kumchagua meya wa Kinondoni kwa sababu hata kisheria, uchaguzi
unatakiwa kuwa robo tatu ya wajumbe ambao walitakiwa kuwa 23, lakini
walikuwa 18, ndiyo maana hata matokeo yalikuwa kura 18,” alisema.
Alidai
madiwani wao walinyimwa fursa ya kuingia manispaa na kuwasilisha
malalamiko yao hivyo hawamtambui Meya wa Kinondoni na kwa sasa hakuna
Meya wa Manispaa hiyo.
0 Comments
on