Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ameendelea na ziara yake ya siku 10 jijini Dar es salaam ambapo Jumatano hii akiwa wilayani Ilala amesema hataweka saini katika nyaraka za ardhi hadi zipitie na Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akizungumza na watumishi wa wilaya ya Ilala
Akiongea na watumishi wa Halmashauri wa Manispaa Ilala, RC Makonda amesema watumishi wengi wa ardhi wasiowaaminifu wamekuwa wakisababisha migogo mingi ya ardhi.
“Kuanzia sasa sitaweka sahihi katika nyaraka zozote za ardhi zitakazofika ofisini kwangu hadi zipitie Takukuru zichunguzwe nimegundua kumekuwa na usanii katika uuzwaji wa viwanja,”alisema.
Makonda aliongeza kuwa anazo nyaraka za watendaji waliokuwa wakifanya uchakachauji huku akiwataka watendaji hao kufanya kazi na watu waridhike.
Alisema wataalamu wa kupima ardhi huacha maeneo na kudai kuwa ni meneo yenye bonde au mto huku baadae wakiyauza au hata kudai vimeisha na baadaye kuyatumia kwa manufaa yao na wakati mwingine maofisa hao kubadilisha mafaili ili wauze kwa watu tofauti.
Kutokana na hali hiyo, aliwatahadharisha maofisa ardhi na mipango miji wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu kwa kutoa taarifa za uongo katika hatua ya upimaji ardhi, uthamini na utoaji fidia kwa wananchi ambao huuza kwa watu zaidi ya mmoja na kusababisha migogoro usioisha kwa wananchi.
“Sitakubali kukaa na watumishi wa vigogo wasioweza kufanya kazi kutatika mkoa huu ,ninafahamu watumishi waliofika Dar es Salaam kwa vimemo ukiuliza ameletwa na kigogo yupo Tamisemi nitawangoa tu,”alisema.
Mkuu huyo bado anaendeleza na ziara yake katika sehemu mbalimbali za wilaya ya Ilala.