Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi namna mtu mmoja alivyofuatiliwa na watu wasiojulikana alipotoka benki kuchukua fedha hadi wakampora mfuko uliokuwa na kiasi cha Sh15 milioni muda mfupi baada ya kufika nyumbani kwake. 

Naibu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Ernest Matiku alisema wana taarifa za tukio la wizi huo uliofanyika Ijumaa iliyopita baada ya mteja huyo  kutoka Benki ya NMB Tabata na wanalifanyia kazi kubaini wahalifu hao. 

Tukio hilo ni moja ya matukio ambayo katika siku za karibuni watu mbalimbali wamekuwa wakiporwa fedha na watu wenye silaha, ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka benki, hali ambayo inajenga wasiwasi juu ya sehemu ambazo majambazi hao hupata taarifa za watu wanaokwenda benki kuchukua fedha. 

Hofu miongoni mwa wateja imezidi kutokana na tukio lililotokea Ijumaa ya wiki iliyopita ambapo majambazi wakiwa na pikipiki mbili walimfuatilia mteja aliyetoka kuchukua fedha benki kiasi cha Sh15 milioni na kumpora mbele ya nyumba yake. 

Akisimulia tukio hilo mwathiri- ka wa wizi huo, alisema alichukua fedha kwenye tawi la NMB Tabata kisha akapanda daladala akaenda kushuka kituo cha Tabata Bima. 

Alisema alipokuwa anaelekea nyumbani kwake hakuwa na shaka, lakini alipokaribia alihisi kuna mtu anamfuata ingawa hakumuona, hivyo aliingia kwenye baa iliyokuwa njiani na kutokea upande wa pili kwa kutumia uchochoro uliokuwapo. 

Alisema baada ya kutokea upande wa pili aliangaza kushoto na kulia hakuona mtu kisha aliamua kuongoza hadi nyumbani kwake. 

“Nilipofika hapo nje kwenye mwembe (umbali wa mita tatu kuingia ndani ya nyumba yake), nikakuta watu wanne wakiwa na pikipiki mbili wamesimama mbele yangu,”alisimulia akiwa nyumbani kwake muda mfupi baada ya kuruhusiwa Hospitali ya Muhimbili alikokuwa anapatiwa matibabu. 

“Wakanitaka niwape fedha ambazo zilikuwa kwenye mfuko nimezishika mkononi. Kabla sijakaa vizuri wakapiga risasi hewani, kutahamaki wakanipiga juu ya goti la mguu wa kulia ikaniparaza, lakini nilikuwa bado nimeng’ang’ania ule mfuko wenye fedha,” alisema. 

Aliendelea kueleza kuwa baada ya kuona hana mpango wa kutoa fedha, wakampiga risasi mguu huo huo chini ya goti ikapasua mfupa mkubwa na kutokea upande wa pili na kumnyang’anya mfuko wa fedha. 

“Hakuna mtu aliyekuwa anafahamu suala hilo zaidi ya mimi mwenyewe,”alisema huku akiugulia maumivu.