RAIS John Magufuli jana aliwapokea marais wawili, Edgar Lungu wa Zambia aliyewasili kwa ziara ya kiserikali na Idriss Deby wa Chad aliyekuja kikazi.

Tofauti na Lungu ambaye ziara yake ilifahamika tangu wiki iliyopita, ujio wa Rais wa Chad ulikuwa wa ghafla na hata serikali ilitoa taarifa ya ujio wake jana saa chache kabla ya kuwasili nchini kiongozi huyo ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Wote wawili baada ya kuwasili nchini walipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride na ngoma za asili.

Licha ya kupokelewa na Rais Magufuli, viongozi wengine waandamizi wa Serikali pia walishiriki kwenye mapokezi ya viongozi hao. Rais Deby aliwasili saa 8 mchana na kulakiwa na Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mwenzake Lungu aliwasili saa 11.20 alasiri na kulakiwa na Rais Magufuli na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Ratiba ya ziara yao inaonesha kuwa kila mmoja atafanya mazungumzo Rais Magufuli katika Ikulu ya Dar es Salaam. 

Shughuli za Lungu 
Ratiba ya Rais Lungu inaonesha leo asubuhi atatembelea ofisi za Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo la ubia baina ya nchi hizo.

Baadaye atazuru pia Shirika la Bomba la Mafuta la Tazama, ambapo atatembelea mitambo ya kusukuma mafuta, pamoja na matangi ya kuhifadhi mafuta ya Tazama vyote vilivyopo eneo la Kigamboni. 

Baada ya ziara hizo za asubuhi, Lungu na ujumbe wake watafanya mazungumzo rasmi na Rais Magufuli, pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Tanzania.

Mazungumzo hayo yatafanyikia Ikulu kuanzia saa 5:00. Marais hao wawili pia watashuhudia utiaji saini wa Makubaliano na Mikataba mbalimbali minne (4) ya ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania kwa upande mmoja na Serikali ya Zambia.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilifafanua kuwa mikataba hiyo inahusu kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano uliopo baina ya nchi hizo. Katika ratiba hiyo, leo jioni Rais Lungu atahudhuria dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa kwa heshima yake na Rais Magufuli. Dhifa hiyo itafanyika Ikulu kuanzia saa 12;30 jioni.

Aidha, kesho Rais Lungu atatembelea Bandari ya Dar es Salaam ambapo atajionea shughuli mbalimbali za upokeaji na upitishwaji wa mizigo bandarini hapo.

Baadaye atafanya ziara fupi kwenye Kampuni ya kusafirisha mizigo inayomilikiwa na Serikali ya Zambia inayojulikana kama Zamcargo, kisha ataelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ambako ataagwa rasmi na mwenyeji wake Rais Magufuli kurejea nchini kwake Zambia.

Katika taarifa hiyo ya Mambo ya Nje inaeleza kuwa ziara ya Rais Lungu inatarajiwa kutoa fursa ya kuzidisha uhusiano na kukuza ushirikiano ili kuongeza ufanisi wa Reli ya Tazara ambayo ni mhimili na kiungo muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa Tanzania na Zambia, lakini pia na kwa nchi nyingine majirani za ukanda wa kusini na kati mwa Afrika za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zimbabwe na Malawi.

Pia eneo lingine litakuwa ni kukuza ushirikiano katika matumizi ya bomba la Tazama ambalo lilijengwa mwaka 1968 kwa lengo la kutoa njia nafuu ya kusafirisha mafuta ghafi kwenda nchini Zambia na hivyo kuiepusha nchi hiyo na athari za kupanda kwa bei ya mafuta. Hata sasa umuhimu wa bomba hilo bado upo.

Eneo lingine litakuwa ni ushirikiano katika matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa muda mrefu Zambia kama nchi ambayo haina bandari imekuwa ikitumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yake. Kwa sababu za kiuchumi na za kihistoria, nchi hiyo imeendelea kuwa mdau mkubwa katika matumizi ya bandari hiyo.

Rais Deby
 Taarifa iliyotolewa na serikali inaonesha Rais Deby ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na watapata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Ukanda wa Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika kwa ujumla.

Deby amefuatana na mkewe, Hinda Deby, Moussa Faki Mahamat ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje, Mtangamano wa Afrika, na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chad na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Chad.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dkt John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake  Rais wa Jamhuri ya Chad Mhe Idriss Deby Itno mara  baada ya kiongozi huyo kuwasili katika uwanja wa  ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Novemba 27, 2016
 Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu akisalimiana na mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali za Afrika nchini mara tu baada ya kupokewa na mwenyeji wake Rais Dkt John Magufuli katika uwanja wa  ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Novemba 27, 2016.