Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa  kumkamata mtuhumiwa wa utapeli anayejulikana kwa jina la  Wilfred Masawe (36) ,  mkazi wa  Buza, Temeke jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi Mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu mbalimbali kutapeli zikiwemo kujitambulisha kama kiongozi wa serikali kwa kutumia mtandao wa Whatsapp,  huku akieleza kuwa yupo nje ya nchi na kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na unamuhusu na hivyo alikua akitoa maelekezo kwa watendaji wa serikali waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha mwili wa marehemu na gharama za mazishi.

Taarifa hiyo pia imesema mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu ya kujifanya kiongozi mkubwa wa dini ya kikristo (Askofu) na kuwaambia waumini na viongozi mbalimbali kuhusu maandalizi ya makongamano ya kidini kwa lengo la kuwaomba michango kuweza kufanikisha makongamano hayo.

Baadhi ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na kuwatapeli viongozi wa serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma, wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini.

Aidha, matukio yote hayo alikuwa akiyafanya peke yake na alikuwa akiyaendesha kwa mawasiliano ya njia ya ujumbe mfupi (SMS) bila kuzungumza kwa simu.

Jeshi la Polisi linakamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
***