Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameitaja rushwa kama changamoto sugu ambayo bado inaendelea kulitafuna taifa la Tanzania katika miaka yake 55 ya Uhuru.

Rais Magufuli ameitaja changamoto hiyo leo akati akiwaongoza watanzania katika maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru wa Tanzania Bara ikiwa ni mara ya kwanza tangu aingie madarakani na kutaja changamoto nyingine kuwa ni tatizo la ajira pamoja na umasikini.

Akizungumza katika hotuba yake ya shukrani katika maadhimisho hayo ambayo yamefanyika katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam, Dkt. Magufuli, amesema kuwa serikali yake itaendelea kupambana na vitendo na rushwa na ufisadi, kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo.

Aidha Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa serikali itahikisha kuwa inaondoa uonevu hasa kwa wananchi wanyonge ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili ili kila mtanzania aweze kufaidika na matunda ya nchi yake.

Maadhimisho hayo ambayo kwa mujibu wa Rais Magufuli ndio ya mwisho kufanyika Jijini Dar es Salaam na kuanzia mwakani yataadhimishwa Dodoma, yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu na serikali pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali zenye uwakilishi hapa nchini.