Header Ads Widget

SIMULIZI YA KUSISIMUA | MIMBA YA JINI | SEHEMU YA TANO


 SASA ENDELEA..

Mmh! Sijui...halafu kwa nini hukufurahia uamuzi wa mkeo?”
“Nimefurahi ndiyo maana tumekubaliana kutanguliza mtoto wa kike.”
“Si kweli Mustafa, moyoni hujafurahia uamuzi wa mkeo kwa kulazimisha kutangulia mtoto wa kike kitu kitakachompa matatizo mtoto atakayezaliwa.”
“Kwa nini?” Mustafa alishtuka.
“Kuukunja moyo wako wakati wa tendo la ndoa tofauti na siku zote. Mimba iliyoingia umeitia sumu.”
“Sumu?” Mustafa alishtuka.
“Ndiyo, ili kuiondoa unatakiwa kuukunjua moyo wako bila hivyo mtoto atakuwa na matatizo.”
“Nimekuelewa.”
“Basi mi nikuache ufanye kazi.”
“Nashukuru ila nilikuwa na hamu sana ya kuonana na wewe.”
“Usiwe na wasi Mustafa utaniona mpaka utanichoka kwanza tumalize tatizo linalowakosesha
raha kwa muda mrefu.”
“Asante, nitakusuburi.”
Mustafa alikata simu na kujikuta akiwa katika mawazo mengi juu ya mtu anayejiita Shehna. Alijiuliza ni nani mtu anayeyajua maisha yake kiundani pia kujua hata mambo yaliyojificha bila kumwambia.
“Huyu mwanamke atakuwa nani...mmh! au...ha...hapana siyo lazima atakuwa mganga tu siyo jini.”
Mustafa aliendelea kuwaza juu ya kauli tata za Shehna ambazo hakuelewa nini hatima yake. Alijiuliza alijuaje kama kitendo cha mkewe kulazimisha mtoto wa kike wakati yeye alitaka wa kiume kitu ambacho alimkubalia kwa shingo upande yeye alifanya siri lakini Shehna alitambua na kumtisha kuhusu ujauzito ambao yeye alisema uliingia siku ile usiku.
Alijiuliza sumu hiyo ni sumu gani ambayo inaweza kuleta matatizo katika ujauzito ule na moyo wake ataunyoosha vipi. Kuingia kwa sekretari wake kulimkatisha mawazo yake.
“Bosi vipi naona upo mbali?” Sara alisema akiwa ameshika faili mkononi.
“Kawaida tu.”
Sara alimpa kazi aliyomuagiza kuifanya, baada ya kumpa alimuuliza.
“Jana nilisahau kukuuliza mlikwenda Mbagala?”
“Sara tumetoka hapa saa ngapi?”
“Kweli, jana kazi zilitushika, kwa hiyo wifi alienda peke yake?”
“Hakwenda ila mwisho wa wiki atakwenda.”
Sara alitoka na kumuacha Mustafa akiwaza na kuwazua aliyoelezwa na Shehna.
****
Jioni wakati Mustafa anajiandaa kurudi nyumbani alipokea simu toka kwa mkewe.
“Haloo mpenzi,” alipokea kwa madaha kama kawaida yake anapopigiwa na mkewe.
“Mume wangu yupo wapi?” mkewe alizungumza sauti ya mtu anayeumwa sana.
“Mke wangu mbona unaongea hivyo?” sauti ya mkewe ilimshtua.
“Na...na...u...mwa.”
“Nini?” Mustafa alitaharuki.
“Na...na...,” sauti ilinyamaza ghafla na kusikia kishindo upande wa pili.
Mustafa alijikuta akitaharuki na kutoka mbio ofisini kuelekea nje kwenye gari lake ili awahi nyumbani kujua mkewe alipatwa na nini. Alimpita sekretari wake aliyekuwa katika maandalizi ya kuzima vyombo vya umeme ili watoke na bosi wake.
Alishangaa bosi wake akitoka mbio kuelekea nje bila kumsemesha, Sara aliacha kazi na kumfuata ili ajue kulikoni. Alimuona akielekea kwenye gari lake akiwa kama amechanganyikiwa, alimkimbilia na kumuuliza:
“Bosi vipi?”
“Sara hebu subiri,” alisema huku akiwasha gari.
“Bosi kuna nini mbona mbiombio kwenye gari au kuna kitu cha kutisha kimetokea ofisini?” Sara alizidi kuhoji.
“Sara niache kwanza,” Mustafa alisema huku akiwasha gari na kuliondoa kwa kasi kuelekea getini na kumpigia kelele mlinzi afungue.
Mlinzi alifungua haraka, Mustafa alilitoa gari kwa kasi kwa kuliingiza barabarani bila kuangalia na kuelekea nyumbani.
Mlinzi alimfuata Sara na kumuuliza:
“Vipi! Kuna nini?”
“Hata najua! Nimemuona akitoka ofisini mbio hata sijui kapatwa na nini?” Sara naye alikuwa amepatwa na mshangao.
“Hukumuuliza?”
“Majibu yake hayaeleweki! Kila nilipomuuliza majibu anajua mwenyewe, kaacha vitu vyake vyote vya muhimu koti, lap top.”
“Mmh! Basi kuna kitu kimempata si bure.”
“Nina wasiwasi kuna kitu kimemtokea ofisini.”
“Twende tukaangalie.”
“Nani aingie ofisini? Toka juzi Bosi simwelewi mambo yake, nina wasiwasi bosi anataka kurukwa na akili,” Sara alisema.
“Mmh! Hapana, asingeweza kuendesha gari vile.”
Wakati wakijadiliana yaliyomtokea bosi wao, Mustafa alikuwa akiwaza nyumbani na kushindwa kuelewa nini kilimpata mkewe ambaye muda mfupi uliopita alizungumza naye akiwa katika afya njema.
Alipofika nyumbani kwake alisimamisha gari lake nje ya nyumba yao na kukimbilia ndani bila kufunga mlango wa gari. Alipoingia ndani alishtuka kumkuta mkewe amelala chini akiwa amepoteza fahamu.
Alijaribu kumwita lakini hakuitikia, alimbeba na kutoka naye nje ili amuwahishe hospitali, alimuweka siti ya nyuma ya gari na kufunga mlango.
Naye alizunguka upande wa pili na kuingia ndani ya gari. Alipowasha gari liligoma kuwaka, alishangaa. Alipoangalia kwenye geji ya mafuta ilimshtua kuona mafuta yalikwisha.
“Shit,” alisema kwa sauti huku akipaga ngumi kwenye gari.
Mara simu yake iliitaka, huku akivuja jasho kutokana na tatizo la mkewe. Alijifuta kwa shati jasho lililokuwa likimvuja kama maji kisha aliitazama simu na kuona aliyepiga ni Shehna.
“Haloo,” alipokea pumzi zikiwa juu.
“Mbona hivyo?” sauti ya Shehna ilionesha kushtuka.
“Nina tatizo.”
“Tatizo gani tena Mustafa?”
“Mke wangu yupo hoi hata sijui anaumwa nini?”
“Mmh! Isiwe mimba?”
“Mimba?” Mustafa alishtuka.
“Eeeh, unashtuka nini?”
“Mimba hiyo imeingia lini?”
“Jana.”
“Acha utani, hakuna mimba inayoweza kuingia mara moja na kuanza kumsumbua mtu.”
“Mustafa kila mimba ina uingiaji wake.”
“Basi yote nitayajua hospitali.”
“Unampeleka hospitali ili iweje?”
“Ana hali mbaya sana, kwanza sijui kama mzima.”
Kauli ile ilimfanya Shehna aangue kicheko kitu kilichomshtua Mustafa na kuhoji.
“Mbona unacheka?”
“Nani alikuambia mimba ugonjwa?”
“Shehna una uhakika gani kama ni mimba?”
“Uhakika ninao, mrudishe mkeo ndani kwa vile haumwi.”
“Hapana siwezi kufanya hivyo lazima nimpeleke hospitali.”
“Haya fanya unavyotaka, lakini usinitafute wala tusilaumiane,” Shehna alitoa kauli ya kitisho.
Kauli ile ilimshtua Mustafa na kumfanya ajiulize Shehna ana maana gani.
“Shehna ulikuwa unataka nifanyeje?” ilibidi awe mpole.
“Mrudishe kwanza ndani.”
“Kisha?”
“Mrudishe kwanza.”
“Sawa.”
Mustafa alimchukua mkewe na kumrudisha ndani akiwa katika hali ileile ya kupoteza fahamu. Baada ya kumlaza kwenye kochi alichukua simu ili kuwasiliana na Shehna.
Alipochukua simu alikuta bado ipo hewani aliita.
“Haloo Shehna.”
“Abee Mustafa.”
“Tayari.”
“Kile kichupa cha manukato kipo?”
“Sijui.”
“Kiangalie kama kipo kisha chukua maji kwenye sahani ya bati nyeupe kiweke kisha mpake kichwani. Akiamka mpe anywe na mengine mpake tumboni.ITAENDELEA.............!!! 

Post a Comment

0 Comments