Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu kufuatia kifo cha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Peter Kakamba kilichotokea tarehe 30 Novemba, 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema anaungana na askari wote wa Jeshi la Polisi, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo cha SACP Peter Kakamba katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

“Natambua mchango mkubwa alioutoa Marehemu (SACP) Peter Kakamba katika Jeshi la Polisi na katika jukumu kuu la ulinzi wa raia na mali zao, kwa hakika tumempoteza kiongozi aliyekuwa akifanya kazi zake vizuri” amesema Rais Magufuli.

“Nakuomba IGP Ernest Mangu unifikishie salamu nyingi za pole kwa familia ya marehemu, askari na wote walioguswa na msiba huu na sote tumuombee Marehemu (SACP) Peter Kakamba apumzishwe mahali pema peponi, Amina” Amemalizia Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam