WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametaka apewe taarifa kuhusu taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) wanaohamasisha au kutangaza ndoa za jinsia moja nchini ili azifutie usajili mara moja.

Aidha ametaka kutajwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria kwa kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinapigwa vita dunia nzima.

Nchemba aliyasema hayo jana mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na taasisi za Kijeshi za mkoa huo zikiwemo Uhamiaji, Polisi, Magereza na Zimamoto juu ya kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Alisema kuwa taasisi hizo hazifai kwani zinafanya kazi ya laana ambayo ni kinyume cha maadili ya Kitanzania na hazistahili kuendelea kufanya kazi kwa upotoshaji huo.

“Leteni majina ya taasisi hizo ili tuzifute kwani hazistahili kuendelea kufanya jambo hilo ambalo ni laana na halipaswi kufumbiwa macho ndani ya jamii,” alisema Nchemba.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na magari.

Mushongi alisema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto hizo wamekuwa wakikabiliana na uhalifu kwenye mkoa huo ambao umekuwa kimbilio la wahalifu kutoka mikoa jirani ya Dar es Salaam.