Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Afrika na Korea unaotarajiwa kufanyika nchini Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba, 2016 mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano huu ambao umeandaliwa na Serikali ya Korea kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika una lenga kukuza ushirikiano pamoja na kuandaa maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Korea na mataifa ya Afrika katika miaka mitatu ijayo.
Tanzania ni moja ya nchi nne (4) za Afrika ambazo Korea imezichagua kuanzisha mahusiano ya kimkakati “strategic partnership” yatakayozifanya nchi hizo kupewa kipaumbele katika kupokea misaada na mikopo nafuu kutoka Korea katika kipindi cha miaka mitano ijayo kati ya 2016 hadi 2020.
Katika kipindi hicho Tanzania itapokea kiasi cha dola za Kimarekani milioni 300 ikiwa ni asilimia 17.1 ya msaada utakaotolewa Barani Afrika, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza Barani humo kupata msaada wa Jamhuri ya Korea.
Pamoja na ushiriki kwenye Mkutano huo, imependekezwa ufanyike mkutano baina ya Tanzania na Serikali ya Korea kuzungumzia masuala ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili. 

Aidha, ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa Afrika na Korea ni fursa muhimu ya kukuza mahusiano baina ya nchi zetu mbili hususan katika Nyanja ya uchumi. Serikali ya Korea ilitoa ahadi ya kuongeza uwekezaji Barani Afrika hususan katikasekta za nishati, miundombinu na viwanda.
Itakumbukwa kuwa, tayari Jamhuri ya Korea inashirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Mradi wa kuendeleza kilimo cha Mwani Zanzibar wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.6 na Awamu ya Pili ya Mradi wa kuboresha Uchunguzi wa Afya ya Uzazi Jijini Dar es Salaam wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni nne (4).
Miradi mingine ambayo Jamhuri ya Korea inashirikiana na Tanzania ni ujenzi wa Daraja la Selander Jijini Dar es Salaam, Mradi wa Daraja la Kikwete kwenye Mto Malagarasi Mkoani Kigoma na Ujenzi wa Hospitali ya Kimataifa iliyopo eneo la Mloganzila Jijini Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 01Desemba, 2016.