Katika mojawapo ya ishara kwamba rais Kenyatta huenda akaanza kuifanyia mabadiliko serikali yake, rais huyo aliambia chombo cha habari cha Nation kwamba anatafuta viongozi ambao wataunga mkono ajenda yake serikalini.
"Nataka watu ambao hawatopinga ajenda yangu ambayo niliandaa na kuahidi Wakenya. Nataka watu ambao wataunga mkono ajenda hiyo. Na katika demokrasia, iwapo unahisi hufurahishwi na uongozi wa kiongozi wako basi…"
Sentensi hiyo ambayo haikukamilika ilionekana kumaanisha kwamba iwapo viongozi hao wanaoegemea mrengo wa naibu wa rais William Ruto wako tayari kushirikiana tena na kiongozi huyo, muda wao umeisha ama ni mfupi kwa wao kufanya hivyo.
Fukuto ndani ya chama cha Jubilee, nani anayelengwa?
Katika mahojiano yaliopeperushwa moja kwa moja na runinga ya NTV nchini Kenya, kiongozi huyo alionekana kumshutumu naibu wake bila ya kutaja jina lake.
Rais Kenyatta amesema kwamba kuna wengi ambao wamekuwa wakiweka mbele malengo yao ya kisiasa badala ya kuzingatia maendeleo.
''Musikubali malengo yenu ya kisiasa siku ya kesho kuzuia kila unachopaswa kufanya leo. Kile unachofanya leo ndio kitakachoamua ni wapi utakuwa kesho'',alisema kiongozi huyo wa taifa.
Kiongozi huyo alikuwa akizungumza kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kamati kuu ya chama tawala cha Jubilee ambapo viongozi wanaoegemea upande wa naibu wa rais William Ruto wanatarajiwa kuondolewa.
Matamshi yake yanajiri siku chache tu baada ya baadhi ya wandani wa naibu huyo wa rais akiwemo aliyekuwa kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen na aliyekuwa naibu wa spika katika bunge hilo Kindiki Kithure kupoteza nyadhfa zao.
Huku akiwa amesalia na miaka miwili katika muhula wake wa mwisho , raia Kenyatta anakamilisha uongozi wake na kuna vitu vitatu anavyoviangazia kwa sasa.
Rekodi yake, alichofanya katika uogozi wake na umoja wa kitaifa. Kwa sasa anasema anataka viongozi ambao anaweza kufanya nao kazi na kutimiza ahadi alizowapatia Wakenya wakati alipokuwa akila kiapo katika uwanja wa Kasarani.
0 Comments
on