Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezitaka taasisi zote za utoaji haki nchini kushirikiana katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ili zifanikiwe.
Akifungua Kongamano la Wadau la kujadili mapambano dhidi ya rushwa katika mfumo wa utoaji haki jijini Dodoma, Jaji Mkuu wa Tanzania amesema Kongamano hilo ni kielelezo tosha cha ushirikiano wa taasisi za utoaji haki nchini katika vita dhidi ya rushwa.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, umuhimu wa kushirikiana katika vita dhidi ya rushwa ulitambuliwa mwaka 2003 wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipotunga Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya Rushwa (The United Nations Convention Against Corruption) ambao ulianza kufanya kazi tarehe 14 Disemba mwaka 2005.
“Mkataba huu uligusia ukweli kuwa Mhimili wa Mahakama hautafanikiwa katika vita dhidi ya Rushwa endapo utasimamia vita hivyo peke yake bila kushirikiana na wadau na taasisi nyingine”, alisema Jaji Mkuu.
Kuhusu mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Mahakama, Jaji Mkuu alisema mbinu nyingi zimetumika ili kuibua na kupima mitizamo na hisia waliyonayo wananchi juu ya vitendo vya rushwa. Baadhi ya mbinu hizo ni kuwekwa kwa mabango yanayopinga rushwa katika Mahakama zote nchini, kujitathmini kupitia utafiti uliofanywa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya REPOA mwaka 2015 na 2019.
Akifafanua kuhusu utafiti uliofanyika, Prof. Juma alisema ulijikita kwenye maeneo ya uridhishwaji na huduma za Mahakama, upatikanaji wa taarifa muhimu za mashauri na huduma zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania.
Alisema taasisi za utoaji haki hazina budi kuwasikiliza wananchi na kutoa nafasi ili wananchi wazikosoe. “Tusiwazuie wananchi kulalamika kwa kuwa malalamiko yao yanaweza kutufumbua macho kuhusu tatizo la rushwa lililojificha ndani ya taasisi zetu”, alisisitiza Jaji Mkuu.
Kuhusu maboresho, yanayofanywa na taasisi yoyote iliyo katika mfumo wa utoaji haki Tanzania Jaji Mkuu alisema hayatokuwa na maana iwapo suala la rushwa katika vyombo hivyo litafumbiwa macho na pale ambapo wananchi wanaofika mahakamani kupata huduma hawatasikilizwa.
Awali akitoa neno la utangulizi, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alisema jitihada za Mahakama za kuandaa mijadala ya aina hii kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) pamoja na wadau wengine ni kielelezo dhahiri cha dhamira ya dhati ya Mhimili huo katika kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanakuwa endelevu na yanaleta matunda chanya.
Jaji Kiongozi alisema rushwa haiathiri Mahakama peke yake bali mfumo mzima wa utoaji haki ndiyo sababu Kongamano hilo limewashirikisha wadau wote wa utoaji haki ili kuweza kujadili kwa mapana kwa vile malalamiko ya rushwa kutoka kwa wananchi yanaelekezwa kwa wadau mbalimbali wa utoaji haki nchini.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma alisema kuna kila sababu ya kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama licha ya kuwepo changamoto nyingi za upatikanaji wa haki zinazopaswa kushughulikiwa.
Kongamano la wadau kujadili mapambano dhidi ya Rushwa katika Mfumo wa Utoaji haki limewakutanisha wadau wa utoaji haki jijini Dodoma kwa lengo la kujadili changamoto zilizopo, lakini pia mikakati iliyopo ya kukabiliana na rushwa nchini. Baadhi ya taasisi zilizoshiriki ni pamoja na Takukuru, BSAAT, Ofisi ya Mpelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), TLS, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Magereza, na Polisi.
0 Comments
on