POLISI mkoani Rukwa inamshikilia askari Magereza, Cleophas Chapaulinge kwa kosa la kulewa na kupiga risasi hewani akiwa wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga na kusababisha taharuki kubwa kwa wagonjwa na wauguzi.
Kitendo cha askari huyo kilizua taharuki kubwa kwenye wodi namba tisa ya wanawake na watoto, ambapo akinamama walipiga mayowe kwa hofu huku wakikimbia na kujificha kwenye chumba cha muuguzi wa zamu wakiwaacha watoto wao vitandani.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea jana alfajiri.
“Chanzo ni ulevi wa kupindukia tulimpima kipimo kikaonesha kiwango cha ulevi kilikuwa juu kupita kiasi alama zikiwa 300 huku kiwango cha kawaida cha kipimo ni alama kati ya 70 na 40 …. Katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa na bunduki yake ilikuwa na risasi 10,” alisema.
Kamanda Kyando alisema siku ya tukio, askari huyo akiwa na mwenzake walikuwa kwenye lindo akilinda makazi ya Kamanda wa Magereza wa Mkoa, lakini alitoroka lindo na kwenda hospitalini wodi namba tisa, ambako mkewe alikuwa akimuuguza mwanawe aliyekuwa amelazwa hapo kwa matibabu.
Mke wa mtuhumiwa huyo, Theresia Kalonga ambaye naye ni askari Magereza, alikuwa amelazwa na mtoto wao wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 10.
“Mtuhumiwa huyo tunamshikilia huku taratibu za kumkabidhi kwa Kamanda wa Magereza Mkoa wa Rukwa ili aweze kushtakiwa kwa taratibu za jeshi lao kabla ya kufikishwa kwenye mahakama za kiraia, zinaendelea,”alisisitiza Kamanda Kyando.
Akizungumza hospitalini hapo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk John Gurisha alisema askari huyo baada ya kuingia wodini, aliweka silaha yake chini akafunua chandarua na kuanza kuzungumza na mwanawe, kisha katoka nje na kufyatua risasi hewani na kutoboa paa.
“Mtuhumiwa huyo alizua kizaazaa kwani askari wetu waliokuwa lindo hapa hospitalini walilazimika kukimbia ili kuokoa maisha yao baada ya kusikia mlio huo wa risasi na kumuona askari huyo akielekea walipokuwa wamekaa,” alisema na kuongeza kuwa askari huyo aliletwa hospitalini hapo na mwendesha bodaboda ingawa hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa, lakini alisababisha taharuki kubwa hospitalini.
“Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliwahi kufika hospitalini hapo na kumtia nguvuni, na bunduki yake ilipokaguliwa ilikutwa ikiwa na risasi kumi,” alisema.
Muuguzi wa zamu wodini humo, Rose Katabi alisema askari huyo alipofyatua risasi akinamama wodini humo walianza kupiga mayowe ya kuomba msaada huku wakikimbia na kuwaacha watoto wao vitandani na kuvamia chumba cha muuguzi kwa ajili ya kusalimisha maisha yao.
“Kwanza kitendo cha kumuona askari huyo akiwa na silaha mkononi, mwili wangu wote ulikufa ganzi nilihisi atatulipua kwa kutupiga risasi za moto …aliiweka silaha yake hiyo chini na kuanza kuzungumza na mwanawe. Aliniuliza kama mtoto wake ameshakunywa dawa, nikamjibu anakunywa dawa mara moja usiku.
“Waliingia walinzi wetu wawili wodini ndipo akaanza, kusema atarudi tena, akatoka nje akiwa katikati ya mlango wa wodini alikoki bunduki yake na kufyatua risasi hewani iliyotoboa paa kisha akaondoka na kutokomea gizani,” alisema.
Kwa upande wa mke wa mshtakiwa huyo, Theresia alisema alipomuona na sare za jeshi na silaha mkononi alimtaka arudi mara moja kazini.
Walinzi waliokuwa kwenye lindo katika lango kuu la kuingia hospitalini hapo kwa masharti ya kutoandikwa majina yao , walidai kuwa askari huyo alifikishwa hospitalini hapo kwa usafiri wa bodaboda.
“Alitutia shaka baada ya kukataa kusimama, kwani alipitiliza moja kwa moja akiwa na silaha mkononi, tulijawa na hofu kubwa tukaamua kumfuata kwa nyuma hadi akaingia wodi namba tisa alikolazwa mkewe na mtoto wake. Lakini tulipomuona akikoki bunduki yake tulilazimika kukimbia na kwenda kujificha ndipo tukasikia mlio wa risasi,” alisema mmoja wao.
0 Comments
on