Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),
Maalim Seif Sharif Hamad anatarajiwa kurejea leo
kutoka ughaibuni alikoenda kwa ziara ya takribani
wiki tatu huku jeshi la polisi likijiandaa kumfikisha
Mahakamani.
Hivi karibuni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest
Mangu alieleza kuwa Jarida la Mashtaka dhidi ya
Maalim Seif liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa
Zanzibar, kutokana na kile alichodai kuwa
aliwachochea wafuasi wake kufanya fujo kupitia
vikao vya ndani vya chama hicho.
IGP Mangu alieleza kuwa uchaguzi wa Oktoba 25
na ule wa Marudio vilifanyika kwa amani na utulivu
lakini matatizo na vitendo vya uvunjifu wa amani
vilianza kuonekana tangu mwanasiasa huyo
aliyegombea Urais kuanza kufanya mikutano hiyo
ya ndani akiwahamasisha wafuasi wake
kutoshirikiana na Serikali iliyopo madarakani.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame
amethibitisha kuwa tayari jalada hilo liko kwa DPP
na kwamba upelelezi unaendelea.
Akizungumzia mpango huo wa Jeshi la Polisi,
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shemeji Mketo
aliwaambia waandishi wa habari kuwa chama
hicho kimekuwa kikisubiri polisi watekeleze azimio
lao hilo ndipo wataeleza msimamo wao.
“Acha wamkamate na sisi tunalisubiri hilo…
wakimkamata ndipo tutasema nini tunafanya,”
alisema Mketo.
Aidha, Mketo alisema kuwa Maalim Seif
atakapowasili atazungumza na waandishi wa
habari kuelezea kuhusu ziara yake, nchi
alizokwenda na mambo aliyoyafanya.