Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw. Javiero Rielo amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania yanaendelea vizuri na kwamba kampuni hiyo imedhamiria kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio.

Bw. Javiero Rielo amesema hayo jana tarehe 24 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na Rais Magufuli kwa lengo la kumpa taarifa juu ya maendeleo ya maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania na unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.

Gharama za mradi wa ujenzi wa bomba hilo zinatarajiwa kuwa takribani Dola za Kimarekani Bilioni 4 na Kampuni ya Total inasema fedha hizo zipo tayari.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli amesema anaamini kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania, Uganda, Kampuni ya Total na nchi jirani.

Amebainisha kuwa pamoja na kwamba Tanzania ipo katika mazingira mazuri ya kutekeleza mradi huo, Serikali yake itatoa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha mradi huo.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi watatu wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Mabalozi waliowasilisha hati zao ni Mhe. Ian Myles – Balozi wa Canada hapa nchini, Mhe. Prasittiporn Wetprasit – Balozi wa Thailand hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi nchini Kenya na Mhe. Harald Gunther – Balozi wa Austria hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi nchini Kenya.

Pamoja na kuwasilisha hati zao za utambulisho Mabalozi hao wameelezea kufurahishwa na mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zao na Tanzania na wameahidi kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Tanzania ili wananchi wa pande zote wanufaike na matokeo ya ushirikiano huo hususani katika uwekezaji na biashara.

Kwa upande wake Rais Magufuli amewahakikishia Mabalozi hao kuwa Serikali yake itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo na ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishawishi zaidi nchi zao na wawekezaji katika nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika ujenzi wa viwanda, uongezaji thamani ya madini, kuendeleza kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa nishati na biashara mbalimbali.

Pia Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi wa Thailand na Austria kuanzisha ofisi za Ubalozi hapa nchini ili kurahisisha na kuharakisha shughuli za kibalozi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
24 Agosti, 2016