Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke kwa tuhuma ambazo hazikuweza kujulikana mara moja.
Taarifa za kukamatwa kwa mbunge huyo, zilianza kusambaa jana jioni, huku zikimuhusisha na mgogoro wa ardhi.
Katibu wa mbunge huyo, Deogratius Salit jana alikiri Waitara kukamatwa na polisi wakati wa ubomoaji wa nyumba za wakazi wa Kata ya Kivule.
Salit alisema nyumba hizo zilibomolewa baada ya kuwapo kwa mgogoro baina ya wananchi wa kata hiyo na Kikundi cha Umoja wa Vijana wa Kikristo Tanzania (UVIKITA) kinachodaiwa kumili eneo hilo licha ya wananchi hao kushinda kesi mahakamani.
Alisema mbunge alifika kwenye eneo hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi kwamba nyumba zao zinabomolewa na Jeshi la Polisi.
“Mbunge alifika katika eneo hilo baada ya kupata taarifa ya kuwapo kwa ubomoaji katika Kata ya Kivule na alifika pale kwa sababu yeye pia ni mwenyekiti wa kata hiyo.
“Baada ya kufika pale alikuta askari wakisimamia ubomoaji huku wakirusha mabomu ya machozi na kuwatawanya wananchi, aliwauliza askari kama wana nyaraka zozote za kuvunja nyumba hizo, ndipo walimwambia kuwa nyaraka hizo zipo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Chang’ombe” alisema.
Salit alisema wakati wakiwa njiani kuelekea Polisi Chang’ombe, Waitara aliwataarifu kwamba amekamatwa na kupelekwa katika kituo hicho.
Alisema hadi sasa bado hawajajua sababu za kukamatwa kwa mbunge huyo na wanamsubiri wakili wake aitwaye Hekima kwa mahojiano zaidi.
Salit alisema zaidi ya nyumba 200 zimebomelewa na kuwaacha wananchi wa eneo hilo wakiwa hawana mahali pa kuishi.
0 Comments
on