Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda
ameliagiza jeshi la polisi mkoa wa Dar es salaam
kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na
kusiwepo kitu kinaitwa UKUTA ili wananchi
waendelee na kazi zao kama kawaida.
Akizungumza jana na kikosi cha kutuliza ghasia
katika kambi ya Ukonga Jijini Dar es salaam Mkuu
wa Mkoa alisema kwa kuwa askari wanafahamu
sheria wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha
juu ya jambo hilo au maelekezo mengine kwa
kuwa Amiri Jeshi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ameshaagiza
kinachotakiwa ni utekelezaji.
‘’Msisubiri maelekezo yoyote kutoka juu, asiwepo
mtu yeyote akafunga duka kwa sababu ya UKUTA,
nyie ni matrekta hakuna UKUTA unaweza kusimama
mbele yenu, mimi kama Mkuu wa Mkoa ninaamini
hatutakuwa na vurugu kwenye Mkoa wetu na
hatuwezi kuruhusu vurugu kwa kuwa tunajua
madhara ya vurugu’’ Alisema Makonda.
Aidha kwa upande wake Kamanda wa Oparesheni
Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lucas
Mkondya alisema jeshi la polisi lipo vizuri na
vijana wameandaliwa vizuri na wameandaliwa kuwa
tayari siku nyingi na hakuna mtu yeyote
atakayethubutu kufanya UKUTA na watakaofanya
hivyo watazimwa kabla hawajafanya chochote.
Kamada aliwataka wananchi wote Jijini Dar es
Salaam kuto jitokeza kwenye oparesheni UKUTA
kwa kuwa maandamano hayo siyo halali na
watakaojitokeza watapata matatizo yasiyowahusu.
Oparesheni UKUTA ilitangazwa na CHADEMA ikiwa
na maana Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania na
ikatajwa tarehe Mosi Septemba nchi nzima chama
hicho kitafanya mikutano ya hadhara jambo
ambalo limepingwa na serikali kuanzia Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufuatia
wakuu wa mikoa..    .. .