Vyama tisa vya siasa kati ya 22 vyenye usajili wa
kudumu vipo hatarini kufutwa kutokana na
kushindwa kukidhi vigezo na matakwa ya kisheria
yaliyoviwezesha kupata usajili wa kudumu.
Hatua ya kufutwa vyama hivyo, vikiwamo baadhi
visivyo na ofisi za kudumu (vyama vya mfukoni)
itafikiwa ikiwa vitashindwa kujieleza kutokana na
makosa ambayo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa imebaini katika ukaguzi uliofanyika hivi
karibuni Bara na Visiwani.
Jukumu kubwa la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa ni kusimamia, kuboresha, kuendeleza na
kudumisha demokrasia ya vyama vingi hapa nchini
majukumu ambayo yanatokana na Sheria ya Vyama
vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya
Gharama za Uchaguzi Na. 7 ya mwaka 2010.
Majukumu mengine ya ofisi ya msajili ni kusajili
vyama vya siasa na kuvifuta vyama ambavyo
havikidhi matakwa ya sheria hiyo na kusimamia
ugawaji wa ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa
kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza ofisini kwake jana, Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi
alisema uhakiki uliofanywa na ofisi yake katika
vyama hivyo upande wa Bara na Visiwani umebaini
kasoro nyingi zikiwamo za ukiukaji wa masharti ya
usajili.
“Katika uhakiki uliofanywa na ofisi yangu
tumebaini kasoro mbalimbali ambazo kwa mujibu
wa sheria ya vyama vya siasa ni miongoni mwa
vigezo muhimu vinavyoangaliwa ili chama kiwe na
sifa ya kusajiliwa,” alisema.
“Kasoro tulizozibaini ni nyingi na baadhi ya vyama
kutokana na mapungufu waliyo nayo huhitaji kutoa
nafasi tena….unaweza kuvifuta hapohapo.”
Msajili hakutaka kutaja majina ya vyama hivyo
ambavyo tayari vimeandikiwa barua lakini alitaja
makosa kuwa baadhi havina ofisi za kudumu
Tanzania Bara na Visiwani au upande mmoja na
vingine havina anuani ya posta.
“Unakuta chama fulani kina ofisi labda Zanzibar
lakini hakina ofisi Bara,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema vyama vingine havina viongozi wa kitafa
kutoka pande mbili za Muungano na pia havina
bodi ya wadhamini iliyosajiliwa kwa Wakala wa
Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) kama sheria
inavyohitaji.
Katika ukaguzi huo, Msajili alibaini pia kasoro
nyingine kuwa ni kukosekana kwa orodha ya
wanachama wa chama husika jambo alilosema
nalo ni muhimu kila chama kuwa na orodha ya
idadi ya wanachama wake.
Vilevile, baadhi ya vyama hivyo vimeshindwa
kuonyesha akaunti ya fedha ya chama hali inayotia
shaka namna vinavyojiendesha.
0 Comments
on