Mvutano kuhusu maelezo ya mlalamikaji katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, baina ya mawakili wa upande wa  mashtaka na upande wa utetezi ulikwamisha usikilizwaji wa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anadaiwa kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Anadaiwa kuwa Juni 28, mwaka huu, Lissu akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa kauli za uchochezi kuwa:
“Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya kidiktekta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikitekta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani ya giza nene.’’

Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa leo kwa upande wa mashtaka kuanza kutoa ushahidi.Wakili wa Serikali Bernard Kongola aliieleza mahakama kuwa walikuwa na mashahidi wawili ambao aliwataja kuwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Kimweli na Staff Sajenti Ndege.

Hata hivyo kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Peter Kibatala aliiomba mahakama wapewe maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo kabla ya kufanya jambo lolote, jambo ambalo liliibua mvutano wa hoja baada ya kupingwa na upande wa mashtaka.

Wakili Kongola aliieleza mahakama kuwa mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, si miongoni mwa mashahidi wao wanaokusudia kuwaita mahakamani.

Pia alisema kuwa kwa mujibu wa sheria hawalazimiki kutoa maelezo hayo ya mlalamikaji kwa mtu ambaye si shahidi.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kibatala alidai kuwa taarifa ya huyo mlalamikaji ndio chanzo au iliyosababisha kesi hiyo na kwamba iwapo watamleta au hawatamleta lakini maelezo yake ni sehemu ya kesi hiyo.

Alidai kuwa hata mashtaka yaliyopo chini ya sheria ya magazeti ni ya muhimu na kwamba hawawezi kujitetea bila kuyaona  na kwamba hata kama upande wa mashtaka hautamuita, wao wataiomba mahakama aitwe kwa lazima.

Hivyo aliiomba mahakama iulazimishe upande wa mashtaka uwapatie maelezo hayo ya mlalamikaji.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Dk Yohana Yongolo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6, mwaka huu, atakapotoa uamuzi, baada ya kupitia vizuri hoja za kisheria za pande zote.