BIASHARA ya Bodaboda imeshamiri katika Jiji la
Dar es Salaam lenye wakazi zaidi ya milioni nne.
Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba helmeti
kupunguza kwa asilimia 69 hatari ya mwendesha
pikipiki kuumia kichwa pale apatapo ajali, na
kapunguza kifo kwa asilimia 42, uvaaji wa helmeti
kwa madereva na abiria wao bado ni kitendawili.
Kamanda wa Usalama Barabarani Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP), Awadhi Haji anasema wameshatoa elimu
ya kutosha kwa waendesha pikipiki ili wahakikishe
wanavaa kofia ngumu pamoja na abiria wao wakati
wanapopanda pikipiki.
"Watakaokaidi agizo tutawakamata madereva na
abiria wao na kuwafikisha mahakamani. Huko
wanaweza kutozwa faini inayoanzia Sh 300,000 au
kufungwa jela kati ya miezi sita au mwaka mmoja
kutokana na sheria ya Sumatra," anasema
kamanda Haji.
Polisi wameamua kufanya hivyo kutokana na faini
ya Sh 30,000 chini ya sheria ya usalama barabarani
kutowaogopesha madereva wengi wa pikipiki.
Ndiyo maana sasa uamuzi ni kuwapeleka
mahakamani.
"Huko tunawashitaki chini ya sheria ya Sumatra na
operesheni hii tunaifanya kwa kushirikiana na
Sumatra wenyewe," anasema ACP Haji.
Gasper Athony wa Chuo cha Future World
kinachotoa mafunzo kwa madereva wa pikipiki
kwa kushirikiana na Chuo cha Mafunzo Stadi
(Veta), anasema zimethibitisha kwamba wapanda
pikipiki wasiovaa helmeti wanapoanguka
wanaumia zaidi kuliko wale waliovaa helmeti.
"Idadi ya waliojeruhiwa kichwani wakati wamevaa
helmeti ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watu
waliojeruhiwa kichwani wakiwa hawakuvaa helmeti.
Kofia hizi ni muhimu kwa dereva na abiria wa
Bodaboda," anasema Antony.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka
2015 inaielezea Tanzania kwamba usimamizi wa
vihatarishi vya uvaaji wa helmeti hapa nchini
unatekelezwa alama 4 kati ya alama 10.
Hii maana yake ni kwamba Mamlaka
zinazosimamia usafiri hapa nchini hususan Jeshi la
Polisi na Sumatra zinatekeleza kwa kiwango cha
chini katika kuhakikisha sheria zinafuatwa na
waendesha Bodaboda linapokuja suala la uvaaji
wa helmeti.
Kwa mujibu wa Antony, ambaye ni mkufunzi wa
madereva wa Bodaboda, uvaaji wa helmeti
unapunguza kujeruhiwa kichwani mara tatu.
"Sehemu ngumu ya nje inazuia kupenya kwa kitu
chochote na sehemu ya ndani ya kofia hiyo
inasaidia kupunguza mgandamizo. Hali kadhalika,
helmeti nyingi zina sehemu ya kukinga macho
dhidi ya vumbi, upepo na kuzuia wadudu
wanaoruka, hivyo dereva kuendesha pikipiki bila
kuvaa helmeti anaweka maisha yake na ya abiria
katika hatari kubwa," anasisitiza Antony.
Kuna aina nne za helmeti na ya kwanza ni Full
Face ambayo inafunika uso wote, pili ni aina ya
Motor Cross ambayo nayo inafunika kichwa chote
pamoja kidevu.
Aina ya tatu ni Modula ambayo inafunika kichwa;
lakini inakuwa na kioo cha kufunua na ya mwisho
ni Open Face ambayo inafunika kichwa lakini haina
kioo mbele.
Robert Mnyambe, mmoja wa madereva wa
bodaboda mjini Morogoro, anakiri kwamba
madereva wengi wa pikipiki hawapendi kuvaa
helmeti kwa madai kwamba uvaaji wa kofia hiyo
ngumu unapunguza uwezo wa kuona na kusikia
vizuri hivyo kusababisha ajali nyingi.
Kwa upande wa abiria, Mnyambe anasema wengi
wa abiria; hasa wanawake hawataki kuvaa helmeti
kwa sababu mbalimbali.
Kuna madai ya kuogopa kuchangiana jasho kwa
vile zinavaliwa na abiria wengi. Kubwa zaidi ya
madai ya abiria wanawake ni eti kwamba helmeti
zinavuruga nywele zao ambazo wanatumia
gharama kubwa kuzitengeneza.
Mfano mzuri ni Neema Wema mkazi wa Dar es
Salaam, yeye hukataa kuvaa helmeti eti kwa kuwa
anahofia kuambukizwa magonjwa ya ngozi
kutokana na kofia hizo kutumiwa na abiria walio
wengi.
"Kofia za hawa bodaboda hawazifanyii usafi.
Zinanuka. Ndio maana sivai," anasema Neema na
kuongeza, “Dar es Salaam ni joto kali, ukiivaa
kofia hii lazima tu utaivua maana inaleta joto na
hiyo kuwa na harufu kali."
Dereva mwingine wa bodaboda, James Kemege,
na ambaye anafanya biashara hiyo kwa mwaka wa
tatu sasa anasema: “Mimi nina helmeti mbili ya
kwangu na abiria. Lakini abiria wengi hawataki
kuvaa helmeti hasa wanawake kwa madai kuwa
nywele zao zinaharibika pia wanadai zina uchafu.”
Kemege anasema abiria wake wanadai helmeti
zinaambukiza ugonjwa wa ngozi, mba. Anaasema
wanadai wanaogopa kuambukizwa magonjwa ya
ngozi kutokana na kofia hiyo kuvaliwa na watu
wengi. Kwa mawazo yake Kemege, serikali
iwachukulie hatua abiria wanaokataa kuvaa helmeti
ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.
"Sisi madereva tukikosea tunapelekwa
mahakamani. Iwe vivyo hivyo pia kwa abiria. Na
watozwe Sh 50,000 wanapokutwa na hatia sawa
na dereva."
Lakini, Anneth Mwakajumba anasema abiria wengi
hawavai kofia ngumu kwa sababu hakuna
ufuatiliaji kutoka kwa polisi jambo ambalo abiria
wanaona sio jambo la lazima kuvaa hiyo kofia.
"Sijawahi kuona polisi inamkamata mwendesha
bodaboda ambaye hajavaa helmeti au abiria
aliyekamatwa kwa kupanda bodaboda bila kuvaa
helmeti. Kwa kuwa hakuna ufuatiliaji ndio maana
watu wengi wanapuuzia kuzivaa, lakini polisi
wakikomaa abiria tutavaa tu kwa lazima maana ni
kwa manufaa ya maisha yetu," anasema Anneth.
Dk Mariam Kalomo, wa Kitengo cha Tiba, Wizara
ya Afya, anaeleza kofia ngumu zinapovaliwa na
abiria mbalimbali zinaweza kuambukiza magonjwa
ya ngozi kama malengelenge, fungasi na seabies.
"Sisi madaktari tunawashauri wateja wa bodaboda
wawe na tabia ya kununua kofia zao kama
hawataki kuambukizwa hayo magonjwa. Lakini pia
ni afadhali maambukizi kwa kuwa yanatibika kuliko
upate ajali ambayo inapelekea kifo," anasema Dk
Kalomo.
Hata hivyo, hakuna takwimu za watu waliougua
magonjwa ya ngozi kwa kuvaa helmeti.
Mkurugenzi wa Global Helmet Vaccine Initiative
(GHVI), Alpherio Nchimbi, anasema utafiti
uliofanywa na na taasisi yake katika mikoa ya
Tanga, Morogoro na Dar es Salaam unaonesha
kuwa wanaume wengi wanavaa helmeti kuliko
wanawake.
"Wanaume wanaovaa helmeti ni zaidi ya mara nne
ya wanawake, hii inadhihirisha kwamba wanawake
hawapendi kuvaa kofia ngumu na hata akipewa na
dereva yuko radhi kuishikilia mkononi,"
anabainisha Nchimbi. Anashauri kwamba wateja
wa bodaboda wapewe elimu ili kila mtu anunue
kofia ngumu na kukaa nayo ndani.
"Kila nyumba ina mwavuli licha ya kuwa sio wakati
wote mvua zinanyesha. Ifikie wakati kila nyumba
iwe na kofia ngumu ili siku itakapolazimu kupanda
pikipiki atumie ya kwake."
Wazo hili linaungwa mkono na abiria Flora
Kamage, kwamba abiria wanaoutumia zaidi usafiri
wa pikipiki waone umuhimu wa kununua kofia zao.
Hii ni itasaidia kujikinga na uchafu na magonjwa ya
ngozi kwa kutumia kofia inayotumiwa na watu
wengi.
Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani Iringa, Patel
Ngereza, anasema dereva wa bodaboda atatakiwa
kuvaa kofia kwa ajili ya usalama wake na abiria.
Kwa maelezo ya Ngereza, sheria ya ulipaji wa
leseni ya bodaboda iliyopitishwa na Bunge mwaka
2011, inapaswa kutumika ipasavyo, ili kuzuia ajali
zinazosababishwa uzembe wa madereva.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani
Mkoani Iringa, Leopold Fungu , anasema polisi wa
kikosi hicho wamekuwa wakiwakamata na
wataendelea kuwakamata madereva wa Bodaboda
na wengine ambao hawazingatii sheria za usalama
barabarani na sheria nyingine za nchi.
Fungu anasema madereva wengi wa bodaboda
wamekuwa wakikamatwa kwa makosa makubwa
saba ambayo ni pamoja na kuendesha chombo
hicho bila kuwa na leseni, wakiwa wamelewa,
hawajavaa helmeti, wamevaa viatu vya wazi,
mwendo kasi na kubeba abiria zaidi ya mmoja na
baadhi kubeba watoto wakati sheria hairuhusu.
Sheria ya usafirishaji wa Pikipikiya Sumatra
hairuhusu mtoto wa chini ya miaka 8 haruhusiwi
kupakiwa kwenye pikipiki bila msaada wa mtu
mwingine.
Licha ya kampuni za kutengeneza helmeti
kutengeneza kofia ngumu kwa watoto, lakini hapa
nchini sheria imenyamaza kuhusu kofia ya mtoto
aliyepanda na kusaidiwa na mzazi. Kamanda wa
Kikosi cha Usalama barabarani mkoani Morogoro,
Boniface Mbao, anakiri kuwa kutovaa helmeti ni
tatizo kubwa mkoani kwake.
Wanachofanya ni kuendelea kuwakamata madereva
wakaidi lakini pia wanatoa elimu.
"Uelewa wa helmeti bado ni mdogo ndio maana
tumekuwa tunafanya operesheni kubwa na
tunapowakamata mbali l ya kuwalipisha faini,
tunawaelimisha umuhimu wa kuvaa helmeti na
faida zake," anasema Kamanda Mbao??