Na Sheila Simba- MAELEZO
Waziri wa Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema kuwa Serikali imeanza kazi ya kupima ardhi  nchi nzima kuanzia mkoani Morogoro.

Akizungumza  katika kipindi kipya cha "TUNATEKELEZA" kinachoandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO na TBC1 ,alisema utekelezaji wa zoezi hilo umeanzia mkoani humo ili kupima maeneo ya wakulima na wafugaji na kutatua migogoro ya ardhi Mkoani humo.

“Serikali tumedhamiria kumaliza migogoro ya ardhi, kutimiza ndoto ya Rais Magufuli ya kuondokana na migogoro ya ardhi isiyo na tija inayosababisha watu kupoteza maisha’’Alisema Lukuvi

 Ameongeza kuwa katika upimaji huo wa ardhi serikali inashirikiana na kampuni binafsi zilizosajiliwa ili kumuwezesha mwananchi anayemiliki shamba,kiwanda ,mkulima na mfugaji mwenye eneo  kupimiwa na kuongezewa thamani.

 “Nakuhakikishia katika kipindi cha miaka 10 kila kipande cha ardhi Tanzania kitakuwa kimepangwa na kupimwa utaratibu mzuri utakao mwezesha kila mtumiaji wa ardhi kutumia eneo lake”alifafanua Lukuvi.

Pia ameeleza suala la kuthibiti bei ya kupima ardhi kwa kushirikiana na wapimaji binafsi katika kumfanya kila mtanzania alipe bei halali ya kupima ardhi.

Aidha amesme kuwa Serikali itaweka ukomo wa kumiliki ardhi ili kuondoa tabia za watu kumiliki eneo kubwa la ardhi bila ya kuliemdeleza kwa muda mrefu.
“serikali itaweka muda wa mtu kumiliki ardhi, haiwezekani mtu mmoja amiliki eneo hata bila kulitumia, tabia hii itafika mwisho.”

Akizungumzia suala la wageni kumiliki ardhi alisema kuwa ni marufuku kwa wageni na wawekezaji kununua ardhi vijijini bila kupitia wizara inayohusika.

“Ni marufuku kwa mgeni au mwekezaji kwenda kijijini kununua ardhi bila kuja kwangu au Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),wakifanya hivyo tutawapa ardhi wawekeze, Pia mtu yeyote anayetaka kujenga kiwanda popote afike ofisini kwangu nitampatia ardhi ndani ya siku saba.”alisema Lukuvi

Ameongeza kuwa  Wizara imetenga viwanja 240 kwa ajili ya Viwanda enoa la Kigamboni ili kutimiz lengo la Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Mbali na hayo Waziri Lukuvi alisema  wananchi wote waliodhulumiwa viwanja Jijini Dar es Salaam kwa makosa ya watendaji wa Serikali wameanza kupewa  viwanja vingine mbadala.

“Naagiza Halmashauri zote ziwapatie viwanja mbadala wananchi ambao walidhulimiwa viwanja vyao kwa makosa ya watendaji.”


MWISHO