WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amewanyooshea kidole maofisa ugani wa mifugo na uvuvi kwa maelezo kuwa wameacha kutimiza majukumu yao na badala yake wanakamata zana haramu za uvuvi, kuuza dawa na kuomba hongo.

Dk Tizeba alisema hayo juzi alipotembelea maonesho ya kitaifa ya mifugo katika viwanja vya maonesho ya wakulima Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho ya Kilimo Kanda ya Kati Nzuguni mjini Dodoma.

Alisema maofisa ugani upande wa kilimo, ufugaji na uvuvi hawawajibiki ipasavyo na wamejibadilisha kuwa wafuatiliaji na wakamataji wa zana haramu za uvuvi, kuuza dawa za mifugo na kupokea hongo.

Pia alisema maofisa nyama wamebaki kuchukua baadhi ya nyama kama hongo na kuruhusu nyama kuuzwa bila kukaguliwa kitaalamu.

Alimuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mary Mashingo kufuatilia utendaji kazi wa Baraza la Usajili wa Maofisa Ugani hao, huku akimtaka pia mwenyekiti wake wa bodi hiyo kumpatia mpango kazi walionao na changamoto zilizopo katika kuwasimamia ili wawajibike vyema zaidi.

Dk Tizeba alisema baraza hilo, mwenyekiti wake wa bodi kuhakikisha kuwa anatengeneza mfumo utakaotoa vibali vya muda utakaowezesha bodi yake kuwapima utendaji wao kwanza kabla ya kuwapatia usajili wa kudumu.

Pia alimuagiza katibu mkuu kutoa maagizo kwa halmashauri zote nchini ili maofisa ugani hao wanapotekeleza wajibu wao chini ya usimamizi wa wakurugenzi wao wawe na mfumo ulio wazi na wenye tija katika kuwahudumia walengwa vizuri zaidi na si kama wanavyofanya sasa kwani hawawajibiki na hawasimamiwi ipasavyo.

Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Gracian Mwesiga alisema inawezekana kuwepo kwa maofisa mifugo wasiotimiza majukumu yao, lakini kwa mwenendo wa sasa wa serikali wanatakiwa kupendekeza na kupitisha sheria itakayompa meno mwenyekiti wa bodi ya usajili wa maofisa ugani ikiwamo kufuatilia utendaji wao baada ya kuwasajili.

“Usimamizi wa maofisa mifugo upo kwenye halmashauri na si katika baraza ambalo kazi yake ni kusajili wataalamu,” alisema Mwesiga.