Maofisa
wa Polisi wamemhoji Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob kabla
ya hajakutana na waandishi wa habari kwa madai kuwa wamepata taarifa
mkutano wake huo ulilenga kumkashifu Rais John Magufuli.
Maofisa
hao waliovalia kiraia walionana na Jacob ofisini kwake na walimruhusu
kuendelea na mkutano huo baada ya meya huyo kuwahakikishia kwamba hana
nia hiyo bali alitaka kutoa ufafanuzi wa baadhi ya masuala baada ya ujio
wa Rais, Kinondoni Jumanne iliyopita.
“Kwa
mara ya kwanza meya anahojiwa, lakini niliwaambia wana usalama lengo
langu ni nini na sipo kwa ajili ya kumkashifu Rais, ila nafahamu vita
iliyopo kati yetu na baadhi ya viongozi,” alisema Jacob.
Pamoja
na ufafanuzi huo, Jacob aliwataka baadhi yao (askari) kushiriki kwenye
mkutano huo wa wanahabari kufuatilia alichotaka kuwaeleza wanahabari na
polisi mmoja alibaki kusikiliza bila kutambulishwa.
Kamanda
wa Polisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda alisema hakukuwa na tatizo lolote
polisi kuwapo eneo hilo, kwani wanafanya shughuli zao za ulinzi na
usalama wa raia na hasa ikizingatiwa kuwa kuna Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Katika
mkutano huo, meya Jacob alitoa ufafanuzi wa yaliyojiri Jumanne
iliyopita wakati Rais Magufuli alipofanya ziara katika manispaa hiyo na
kubatilisha umiliki wa eneo la Magomeni Kota lililokuwa mali ya
halmashauri kuwa ya Serikali Kuu.
Meya
Jacob aliwaambia wanahabari kuwa uamuzi wa Serikali kuchukua eneo hilo
umeisababishia halmashauri yake hasara ya zaidi Sh4.5 bilioni kutokana
na gharama walizoingia.
Katika
eneo hilo, nyumba 644 zilivunjwa mwaka 2011 kwa miadi ya kwamba
zikijengwa upya, wananchi waliokuwa wakiishi hapo wakiwa wapangaji
wangerejeshwa, lakini mradi huo ulichelewa kuanza.
Akiwa
ameambatana na baadhi ya madiwani, Jacob alisema hasara hiyo imetokana
na halmashauri kutumia Sh2 bilioni kumlipa mkandarasi kwa ajili ya
michoro ya eneo litakavyokuwa.
Alisema
pia manispaa hiyo imetoa Sh1 bilioni kwa mkandarasi Gulf kwa ajili ya
kuchora ramani ya ofisi mpya za halmashauri na kusimamia ujenzi wa mradi
huo na kutumia Sh700 milioni kuwalipia kodi wapangaji hao baada ya
kuwahamisha.
“Faida
tuliyoipata ni kwamba wananchi tuliopanga kuwahudumia tayari Rais
amewahudumia. Hatupingi maamuzi ya Serikali, lakini wananchi watambue
kwamba manispaa haina chochote itakachokipata, bali kila kitu kitakuwa
kinafanywa na Serikali Kuu,” alisema Jacob.
Meya
alisisitiza kuwa madiwani wa Ukawa hawapingi uamuzi huo ila baadhi ya
viongozi wanaomzunguka Rais hawamwambii ukweli wa mambo kuhusu mradi wa
Magomeni Kota na kwamba baadhi ya watumishi wa Serikali ndiyo
waliosababisha kufikia hatua hiyo.
“Siku
ile ningepata nafasi hata dakika tatu, ningemweleza Rais Magufuli
ukweli wa mambo wa mradi huu. Lakini kuna baadhi ya viongozi
waliomzunguka waliamua kuninyima nafasi hiyo. "
Hata
hivyo, Jacob alimwomba Rais Magufuli kukutana naye ili amweleze kwa
undani jambo linalomuumiza kuhusiana na masuala ya ardhi yanayoikumbuka
Kinondoni.
Alifafanua
kwamba, Serikali iliyopita na manispaa hiyo ilishaingia mkataba na
kampuni ya Blue Marine ya Romania kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa
Magomeni Kota ambao ulifikia katika hatua nzuri lakini baadhi ya
watumishi wa Serikali waliamua kuweka ‘kauzibe’ na kuipa sifa mbaya
Kinondoni.
“Tulikuwa
tunasubiri utiaji wa saini kutoka Serikali Kuu, lakini baada ya kuona
Kinondoni inaongozwa na Ukawa wameamua kuleta ‘figisufigisu’ za
kuukwamisha,” alisema Jacob.
Katika
ziara hiyo, Rais Magufuli alielezea kusikitishwa kwake na namna tatizo
la wakazi hao lilivyoshughulikiwa na kuwaahidi kuwa Serikali yake
itahakikisha hawasumbuliwi.......