Rais
wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema Serikali imetenga Shilingi
Bilioni 483 kwa mwaka huu kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ambapo
wanafunzi zaidi ya 118,000 watanufaika.
Akizungumza
katika uwekaji wa jiwe la msingi la hostel za Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam leo, Rais Magufuli amesema miongoni mwa hao watakaonufaika,
wanafunzi 93,000 ni wanaoendelea na masomo na wanafunzi takribani 25,000
ni watakaoanza masomo mwaka huu huku akiweka bayana kuwa mikopo hiyo
itatolewa kwa wanafunzi ambao wanatoka kwenye familia masikini.
Rais
Magufuli ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kurekebisha
dosari zilizopo katika mfumo wa utoaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na
upangaji mbaya wa wanafunzi katika vyuo, kutoa mikopo kwa upendeleo,
kutozingatia sifa za mkopaji, kutoa mikopo hewa na kufungua vyuo kabla
ya mikopo ya wanafunzi kutolewa na pia amewaonya wanafunzi kujiepusha na
vitendo visivyofaa wakati Serikali inarekebisha dosari hizo.
"Na
ndio maana wakati mwingine na wabaya wanapitia humo humo, mara fanye
hivi fanyeni vile, wakati wanajua kuwa mkifanya yasiyofaa Serikali
itawafukuza tu ili mkafanyie mambo yenu huko.
"Kwa
sababu huwezi kuwa unahangaika kutafuta fedha za kuwapa mikopo, wakati
huo huo unahitaji kujenga reli, wakati huo huo unahitaji kujenga
barabara, wakati huo huo unahitaji kulipa mishahara, wakati huo huo
unahitaji kutoa elimu bure, wakati huo huo Karagwe kuna njaa, wakati huo
huo watu wanahitaji dawa hospitali, halafu watu wengine wanataka
kukuendesha kana kwamba hela unayokusanya ni kwa ajili yao tu, ni lazima
tuelewane na mimi ninataka kuwaeleza kwa dhati lazima twende katika
njia iliyonyooka, ni bora uwe Rais usiye maarufu lakini utimize
uliyoyaahidi, asitokee mtu wa kukuendesha, ninajua mmenielewa" amesisitiza Dkt. Magufuli.
Dkt.
Magufuli ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kujipanga
vizuri kukusanya marejesho ya mikopo kwa wote waliokopeshwa na bodi hiyo
ambapo mpaka sasa bodi inadai takribani Shilingi Trilioni 2.6.
0 Comments
on