“Hatutatoa
mikopo mwaka huu mpaka hapo tutakapokamilisha kazi ambayo tumeanza
kuifanya ya kupitia upya utaratibu wa utoaji mikopo hiyo ili kuhakikisha
inatolewa kulingana na mahitaji ya sasa ya nchi na kwa wanaostahili,” alisema Dk Shein.
Akizungumza
katika hafla ya utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza
katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne mwaka 2015 na Kidato cha
Sita mwaka 2016, Dk Shein alisema kuwa katika utaratibu wa sasa wapo
waliodanganya kupata mikopo na ambao wamekopeshwa lakini wamekuwa wagumu
kurejesha mikopo hiyo.
Katika
hafla hiyo, ambayo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Usii Gavu, jumla ya
wanafunzi 119 waliomaliza kidato cha nne na wengine 50 waliomaliza
kidato cha sita, walipewa zawadi kwa kupata daraja la kwanza katika
mitihani yao ya taifa.
“Wako
waliokejeli matokeo yenu, lakini ukweli ni huo mko 50 wa kidato cha
tano mliopata daraja la kwanza na wengine 119 mliofaulu daraja la kwanza
mtihani wa kidato cha nne,” alieleza Dk Shein na kuhoji msingi wa kukebehi matokeo hayo.
Aliongeza
kuwa ufaulu wa wanafunzi hao, ni sifa kwa Zanzibar na anaamini kwa
hatua zinazochukuliwa na serikali kuimarisha miundombinu ya elimu pamoja
rasilimali watu kiwango cha ufaulu kitazidi kuongezeka.
“Mnapofanya
mitihani sote tunakuwa na wasiwasi, nyinyi wenyewe, walimu, wazazi na
sisi serikali kwa kuwa tunaelewa kuwa matokeo yoyote yale ni yetu sote
kama ni mazuri ni furaha yetu sote na kama si mazuri ni huzuni yetu
sote,” Dk Shein aliwaambia wanafunzi hao.
Dk
Shein aliwataka wanafunzi hao kujivunia fursa waliyoipata na kuitumia
vyema kujiimarisha kielimu, kwa kuwa haikuwa rahisi kabla ya Mapinduzi
ya mwaka 1964 kuona vijana kutoka familia masikini wanapata fursa za
kuingia sekondari kwa makundi.
“Mmepata
bahati kubwa serikali yenu imeweka mazingira mazuri ya kupata elimu na
haya ni matokeo ya utekelezaji wa ahadi ya Chama cha Afro-Shirazi na
Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amaan Karume ya kutoa elimu
bure itakaposhika madaraka,” Dk Shein alieleza.
Katika
hatua nyingine, Dk Shein ametoa wito kwa walimu wakuu kuhakikisha kuwa
wanasimamia vizuri walimu katika shule zao pamoja na kuwahimiza wakaguzi
wa shule kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Dk Shein alisema;
“kumekuwepo na tatizo la usimamizi maskulini, hivyo serikali
itatengeneza utaratibu wa kuwapatia motisha walimu wakuu na wakaguzi
watakaofanya vizuri kwa kuwa ni dhahiri kuwa walimu wakuu wakisimamia
vyema skuli zao na wakaguzi wakaifanya kazi yao ya ukaguzi kwa umakini
tutapata matokeo mazuri zaidi.”
Katika
salamu zake hizo kwa wanafunzi hao, ambao walisindikizwa na uongozi wa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, pamoja na walimu wakuu wa baadhi ya
shule, Dk Shein aliwataka walimu kuongeza ari ya kufundisha na kwamba
ni heshima na furaha ya mwalimu kuona mwanafunzi wake anapata matokeo
mazuri.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi zawadi Mwanafunzi Mahira Baraka Hamadi wa kidato cha sita Skuli ya Biashara Mombasa Wilaya ya Magharibi Unguja akiwa ni mwanafuzi aliyefanya vizuri katika Mtihani wa Taifa Mei mwaka 2016,hafla iliyofanyika jana Ikulu Mjini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi zawadi Mwanafunzi Mahira Baraka Hamadi wa kidato cha sita Skuli ya Biashara Mombasa Wilaya ya Magharibi Unguja akiwa ni mwanafuzi aliyefanya vizuri katika Mtihani wa Taifa Mei mwaka 2016,hafla iliyofanyika jana Ikulu Mjini Unguja.
0 Comments
on