Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage jana alitofautiana na wamiliki wa malori aliposema upungufu wa mizigo ni tatizo la muda duniani, wakati wafanyabiashara hao wamesema ni vigumu kuwarejesha wenye mizigo waliokuwa wakitumia Bandari ya Dar es Salam ambao wamehamia bandari za Mombasa na Beira.
Waziri
Mwijage alisema hayo wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama cha
Wamiliki wa Malori (Tatoa), alipowaeleza hali ya kupungua mizigo inaweza
kuchukua mwaka na zaidi na kuwataka wafanyabiashara hao kuwa wavumilivu
katika kipindi hiki.
Waziri Mwijage aliwataka wamiliki hao wa vyombo vya usafirishaji kusitisha huduma hiyo kwa sasa hadi hali itakapotengemaa.
“Ushauri
wangu kwenu ni kusimamisha malori yenu na kuyatunza vizuri kwa sababu
mizigo haipo hivi sasa, hali ikirejea muendelee kufanya biashara,” alisema. Alisema kukosekana kwa mizigo ni anguko dogo la uchumi wa dunia ambalo baadaye litaimarika.
“Niwasihi
msiangalie sana muda, inaweza kuchukua mwaka mmoja au zaidi kidogo ya
hapo ili kurudia hali ya zamani, lakini msikate tamaa,” alisema Mwijage.
Waziri
Mwijage alisema kushuka kwa bei ya madini kwenye soko la dunia
kumesababisha nchi kama Zambia na Congo DRC kupunguza mizigo inayopitia
kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema
baadhi ya migodi ya nchi hizo imesitisha uzalishaji na kusababisha
mizigo ya kusafirisha ipungue kwa kiasi kikubwa. Waziri pia alisema
mazao ya biashara yameshuka bei kwenye soko la dunia na hivyo kupunguza
uzalishaji na kuleta athari katika sekta ya usafirishaji.
Lakini
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya NMC Tracking, Natal Charles alisema
itachukua muda mrefu kuwarejesha watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam
kwa sababu waliondoka kwasababu ya ushindani wa kibiashara uliopo kwenye
bandari nyingine.
“Kukosekana
kwa mizigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam ni changamoto kwetu wenye
malori kwa sababu wapo waliokopa benki ili kuyanunua magari hayo na sasa
wako katika hatari ya kufilisika,” alisema.
Alisema pia wako baadhi ya wamiliki wa malori ambao wameshafilisika kutokana na kukosa mizigo.
Kwa
mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari vya nje, moja ya sababu
inayohusishwa na kuathirika kwa usafirishaji wa mizigo duniani ni
kufilisika kwa kampuni kubwa ya meli ya Korea Kusini inayoitwa Hanjin,
ambayo inashika nafasi ya saba katika biashara hiyo duniani.
Kufilisika
kwa kampuni hiyo kumesababisha meli za kampuni hiyo kunyimwa kibali cha
kushusha au kupakia mizigo kutokana na kutokuwa na uhakika wa
kufikishwa inakoelekea, limeandika gazeti la The Guardian la Uingereza.
Katika
hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mwijage aliwashauri wamiliki wa malori
kuangalia aina nyingine ya uwekezaji, kama kujenga viwanda.
“Wekezeni katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kulingana na uwezo na fursa ya kila mmoja wenu,” alisema.
Alisema
anawafahamu baadhi ya wanachama wa Tatoa ambao wameanzisha viwanda vya
maziwa, maji, kutengeneza mabomba na kusaga mahindi ili kupata unga.
“Mwekezaji
makini hawezi kung’ang’ania biashara ya aina moja kwani inapoleta
hasara anaachana nayo na kuendelea na ile inayomletea faida,” alisema.
Hata
hivyo, Mwijage aliwataka Tatoa kupeleka mapendekezo yao serikalini ya
namna ya kuboresha sekta ya usafirishaji huku wakitoa mifano halisi ya
namna ya kuiboresha sekta hiyo.
“Wizara
yangu ndiyo yenye dhamana ya kuboresha wepesi wa kufanya biashara.
“Nileteeni masuala yote yanayowakwamisha nami nitayawasilisha kwenye
mamlaka husika,” alisema waziri huyo.
Alisema
kama malori ya mizigo hayasafiri, biashara ya vipuri itashuka na
matumizi ya mafuta yatashuka na hivyo kuziathiri sekta nyingi.
Alisema malori yamekuwa yakisaidia kuongeza mapato ya Serikali na kutunisha mfuko wa barabara.
Awali,
Mwenyekiti wa Tatoa, Elias Lukumay alisema wamiliki wa malori
wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maeneo ya kuegesha malori wakati
yakisubiri kupakia mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema mara kwa mara wanapoegesha kwenye maeneo ya barabara jirani na bandari hiyo wamekuwa wakikamatwa na kutozwa faini.
==
0 Comments
on