Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imepiga marufuku wanasiasa kutumia nyumba za ibada kwa shughuli za kisiasa Visiwani Zanzibar.
Msimamo
huo wa Serikali umekuja siku chache tangu Katibu Mkuu wa CUF, Maalim
Seif Sharif Hamad, kutumia kila siku za Ijumaa kufikisha ujumbe katika
msikiti atakaoswali.
Akitoa
tamko la Serikali jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohammed Aboud Mohammed alisema Serikali inawaagiza wakuu wa mikoa yote
ya Zanzibar kusimamia utekelezaji wa agizo hilo katika mikoa yao.
“Kwa
taarifa hii Serikali inawaagiza wakuu wa mikoa kupitia kamati zao za
ulinzi na usalama kusimamia utekelezaji wa agizo hili katika mikoa yao,”
alisema Waziri Aboud.
Alisema Serikali imewaagiza wakuu hao wa mikoa kuchukua hatua za kisheria kwa mtu yeyote atakayekiuka agizo hilo.
Waziri
Aboud alisema kwamba viongozi wa dini na kamati zao katika nyumba za
ibada watakaoruhusu wanasiasa kuendesha shughuli za kisiasa
watawajibika kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisema
kwamba hivi karibuni katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi
Unguja katika Misikiti ya Mbuyuni, Kihibnani na Kwabiziredi kumetokea
tabia kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa kupita na kutoa hotuba za
kisiasa katika misikiti hiyo.
Waziri
huyo alisema kwamba shughuli za vyama vya siasa zinaendeshwa chini ya
sheria N0 5 ya mwaka 1992 ambayo imeeleza wazi mipaka na shughuli za
kisiasa ziendeshwe chini ya sheria hiyo.
“Vitendo
vinavyofanywa na viongozi hao wa kisiasa wanaotumia nyumba za ibada
kama majukwaa ya kisiasa wanakwenda kinyume na dhamira ya katiba na
sheria za nchi ikiwemo sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992” Alisisitiza Waziri Aboud.
Waziri
Aboud alisema kwamba shughuli zote za dini ya kiislamu Zanzibar
zinasimamiwa kupitia sheria namba 9 ya mwaka 2001, namba 2 ya mwaka 2007
na namba 3 ya mwaka 1985 zinazoongoza Taasisi mahsusi kama vile Ofisi
ya Mufti, Ofisi ya Mahakama ya Kadhi na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya
Amana.
Alisema
kupitia katiba na sheria , uhuru wa mtu kuabudu dini anayoitaka
umetolewa bila kuingiliwa na itikadi za vyama vya siasa kama
inavyobainishwa na katiba zote mbili ibara ya 19 ambazo zinaeleza
umuhimu wa uhuru wa mtu kuamini dini aitakayo kwa misingi ya kukuza
usalama na amani katika jamii.
0 Comments
on