Kuna uwezekano mkubwa kukawa hakuna bifu kati ya Alikiba na Diamond lakini wapo wachache wanaokuza hilo jambo kwa maslahi yao binafsi. Diamond ameonekana kulipa fadhila kwa Alikiba baada ya kumuombea mashabiki wampigie kura kwenye tuzo ya MTV EMA 2016 akiwa msanii pekee kutoka Afrika Mashariki anayewania tuzo hiyo.
Kiba atachuana na wasanii wengine wakiwemo Wizkid na Olamide wa Nigeria na Black Coffee na Cassper Nyovest wa Afrika Kusini huku mshindi katika hatua ya kwanza ataendelea kwenda kuwania kipengele cha Worldwide Act: Africa/India ambacho mwaka jana alishinda Diamond Platnumz.
Akiongea kwenye kipindi cha D’Wikend Chatshow cha Clouds TV, hitmaker huyo wa Salome amesema, “Nimesikia Alikiba amechaguliwa kwenye tuzo za MTV EMA. Tufute zile zama za kusema kwasababu wewe unam-support Diamond ndio huwezi kumpigia kura Alikiba. Akikosa tuzo hiyo haiji kabisa Tanzania na itaonekana watanzania wote tumeikosa. Kwahiyo tuhakikishe tuna VOTE ili tuirudishe tuzo hiyo nyumbani.”
Alikiba aliwahi kusema kama hivyo mwezi Juni, mwaka huu kwenye kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio alipowataka mashabiki wampigie kura Diamond kwenye tuzo za BET.