Pamoja na hayo, Maalim Seif, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), amesema kuna jitihada alizoziita za mwendokasi za jumuiya ya kimataifa kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Maalim
Seif alisema hayo jana wakati akitoa salamu zake fupi kwa mamia ya
waumini na wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika Msikiti wa
Kihinani, Wilaya ya Magharibi A.
CUF
iko kwenye mvutano wa uongozi kutokana na Profesa Lipumba kushika ofisi
kuu za chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam akisema kuwa
ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho baada ya Msajili wa Vyama vya
Siasa nchini kutoa msimamo na maoni ya ofisi yake kuhusu sakata hilo.
Profesa
Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF Agosti mwaka jana, akipinga chama
hicho kuendelea kuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) baada
ya vyama vinne vinavyounda umoja huo kumpitisha Edward Lowassa kuwa
mgombea wao wa urais.
Hata
hivyo, Juni mwaka huu Profesa Lipumba alimuandikia barua katibu mkuu
akitaka atengue barua yake ya kujiuzulu, lakini Mkutano Mkuu wa chama
hicho ulijadili suala hilo na kuazimia kukubaliana na kujiuzulu na
baadaye Baraza Kuu kupitisha uamuzi wa kumvua uanachama.
Lakini
Maalim Seif, ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi ambao
matokeo yake yalifutwa mwaka jana, anauchukulia mgogoro huo kuwa ni
njama za kuwaondoa kwenye mikakati yao ya kudai haki.
“Nasema
hiyo ya Profesa Lipumba ni ajenda iliyolenga kutuparaganya ili tuondoke
katika mazingira na hima ya kutetea haki yetu iliyoporwa. Lakini
msijali hiyo haitafanikiwa nasi tumefikia pazuri sasa,” alisema.
Katika
hadhira hiyo, Maalim Seif alilaumu juhudi alizoziita za baadhi ya watu
kutumia vibaya mamlaka kutaka kumzuia asiongee na wananchi licha ya kuwa
umma unayo shauku kubwa ya kuhitaji kumsikiliza kila anapopita.
“Najua
zipo kila mbinu na hila za kutaka mimi nisiongee nanyi. Wenyewe
mmeshuhudia hapa msikitini baada ya kubainika nakuja, lakini nasema mimi
ni binadamu na kiongozi, ninayo haki ya kuongea na yeyote
popote.Nitaongea na nitaongea popote pale,” alisema.
Mkwamo wa kisiasa
Alisema zipo juhudi za ‘mwendo kasi’ kuelekea ufumbuzi wa mkwamo wa kisiasa Zanzibar kupitia meza ya jumuiya ya kimataifa.
“Wapi
lilipofikia suala hili ambalo naweza kuliita mwendo kasi? Nasema
limefikia pazuri mno, tulieni wala msiwe na shaka, tumefikia hatua ya
matumaini makubwa,” alisema Maalim, mmoja wa wanasiasa wenye nguvu visiwani Zanzibar.
Maalim
Seif pia alizungumzia suala la Katiba mpya, akisema kumekuwapo na
juhudi za chini kwa chini za kutaka kupiku ridhaa ya wananchi kwa
kuipitisha Katiba Inayopendekezwa kwa lazima.
Mswada wa mafuta
Akizungumzia
muswada wa mafuta na gesi uliopitishwa hivi karibuni na Baraza la
Wawakilishi Zanzibar, Maalim Seif alisema hicho ni kiini macho kwa kuwa
hakuna mabadiliko yoyote hadi sasa juu ya sheria hiyo ndani ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wabunge wazuiwa Mtwara
Katika
hatua nyingine, wafuasi wa CUF wakiongozwa na mbunge wa Tandahimba,
Katani Katani jana walizuiwa na polisi kuendelea na mkutano wa ndani kwa
kile kilichodaiwa ni kuwapo kwa dalili za vurugu.
Wafuasi hao ni wale wanaompinga Profesa Lipumba ambaye anatambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini.
Tukio hilo lilitokea jana wilayani Newala wakati wafuasi hao wakiendelea na ziara yao katika wilaya mbalimbali kanda ya kusini.
Katani
ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi lililomvua Lipumba
uanachama, alisema amesikitishwa na kitendo cha askari kuwaruhusu
kufanya mkutano na saa moja baadaye kwenda kuwatawanya bila kuwaambia
sababu za msingi.
Alisema
kuwa baadhi ya viongozi wa wilaya ya Newala wanaomuunga mkono Profesa
Lipumba walikwenda polisi na kufanya mbinu mkutano huo usiendelee.
“Newala
kuna figisufigisu, tulitoa taarifa za kikao cha ndani polisi na
waliridhia, lakini viongozi wa wilaya wakaenda polisi kwa kushtukiza
kusema kikao kisiendelee kwa hiyo tukafanya kikao cha ndani, lakini ghafla walituvamia wakiwa na bunduki na mabomu ya machozi na kututawanya,” alisema Katani.
Mbunge
huyo alidai kuwa kutokana na tukio hilo, wanaamini tamko la kuruhusiwa
kufanyika mikutano ya ndani lililenga kumpa nafasi Profesa Lipumba na
wanatarajia kutoa tamko leo kwa kuwa walipotaka kufanya kikao walikosa
ulinzi wa polisi.
“Hii
imesababisha kuamini kwamba Profesa Lipumba anatumika, maana inaonyesha
wazi juzi alipokuwa Newala aliruhusiwa kufanya mkutano akiwa na ulinzi
wa polisi, lakini leo (jana) sisi katika ukumbi ule ule mimi nikiwa kama
mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi na mbunge wa kuchaguliwa na wananchi
polisi wameshindwa kutoa ulinzi,” alisema Katani
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa, wa Mtwara, Thobias Sedoyeka alisema walilazimika
kuchukua hatua hiyo kutokana na kuwapo wa dalili za vurugu kutoka pande
mbili, unaomuunga mkono Maalim Seif na mwingine Profesa Lipumba.
“Pande
mbili zina mgogoro kwa hiyo kulikuwa na mvutano pande zote mbili za
Maalim na Profesa. Mimi nimeona kuna dalili ya vurugu na vurugu
zingekuwapo hata wao wangefanya nini,” alisema Sedoyeka.
Katani pia alizungumzia taarifa zinazoenea kwenye mitandao za kukamatwa kwa wabunge wa kusini.
Katani pia alizungumzia taarifa zinazoenea kwenye mitandao za kukamatwa kwa wabunge wa kusini.
“Ni
kweli tulikuwa Nachingwea tukitokea Ruangwa wakati tukisubiri kupata
chakula tukawa tunapata kahawa na wananchi waliokuwapo pale tukawa
tunabadilishana, mawazo lakini kuna watu walitoa taarifa polisi kuwa
tunafanya mkutano wa hadhara na polisi walipokuja tulikwenda kituoni na
kufanya majadiliano na walijiridhisha kuwa kile walichoambiwa hakikuwa
sahihi,” alisema.
Hivi
karibuni, Profesa Lipumba akiongozana na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah
Nachuma alifanya ziara mkoani Mtwara na kukutana na wafuasi wake katika
Wilaya ya Mtwara na Newala akisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha
chama.
0 Comments
on