Salome ya Diamond imezidi kupata heshima kubwa ndani na nje ya nchi na inawezekana ikawa ni tofauti na mwenyewe alivyotegemea. Msanii wa muziki wa asili, Mrisho Mpoto amedai kufurahishwa na wimbo huo kutokana na kuwa na ladha ya Tanzania.

Mpoto amediriki kusema hayo kupitia mtandao wake wa Instagram wikiendi hii huku akiendelea kwa kumpongeza msanii huyo kwa kuutangaza muziki wa Bongo Fleva na kuiletea heshima Tanzania.

“Nassibu kiukweli nimefurahishwa sana na kazi yako ya #Salome imeonyesha ukomavu Mkubwa na team work, kikubwa ukiwa unafanya kazi zenye test ya nyumbani unatupa heshima kama nchi na inakuonyesha wewe ni nani? na nani siyo wewe?,” ameandika Mpoto kwenye mtandao huo.

“Nassibu Mwenda kwao siku zote haogopi Giza, nenda lakini waambie nna kwetu, kama ulivyofanya kwenye Salome. Sisi ni wabantu bwana tunaruhusiwa zaidi ya mmoja, na Mimi ntamtafuta Salome wangu wa ukubwani ashike magoti nisimame kama ngongoti japo nna kitambi ntainama kidogo!!.”

Mpaka sasa video ya wimbo huo imeshatazamwa mara zaidi ya milioni mbili ndani ya wiki moja tangu itoke.