MKURUGENZI
wa kiwanda cha magodoro cha Dodoma Asili Bw. Haidary Gulamali amesema
atawaleta madaktari bingwa 14 kuja kufanya upasuaji wa moyo bure kwa
watoto watakaobainika kuwa na matatizo hayo.
Amesema
madaktari hao ambao wanatarajia kuingia nchini hivi karibuni ataanzia
kutoa huduma hiyo katika hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza na
kisha hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.
Bw. Gulamali ametoa kauli hiyo Jumapili,
Oktoba 2, 2016 wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kiwanda
hicho akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii
mjini Dodoma.
“Mtoto
wangu amefanyiwa upasuaji wa moyo mara sita na Desemba atafanyiwa
upasuaji mwingine nchini India. Nikiwa nchini India nimefahamiana na
kujenga urafiki na madaktari wengi wa moyo kati yao 14 watakuja nchini
na kutoa huduma ya matibabu hayo bure,” amesema.
Mbali
na kupeleka madaktari hao katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,
pia Bw. Gulamali ameahidi kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan
Rugimbana magodoro mapya kwenye hospitali hiyo.
Wakati
huo huo Bw. Gulamali amemkabidhi Waziri Mkuu magodoro 200 yenye thamani
ya sh. milioni 10 kusaidia wananchi waliathirika na tetemeko la ardhi
lililotokea Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 wengine
440 walijeruhiwa.
Pia
tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081
zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata
uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
Waziri
Mkuu alishukuru Bw. Gulamali kwa msaada huo na kuahidi kuwa Serikali
itahakikisha magodoro hayo inayafikisha Kagera kwa walengwa kama
ilivyokusudiwa.
Pia
Waziri Mkuu alimpongeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho kwa uamuzi wake wa
kuleta madaktari bingwa wa moyo kutoka India watakaotoa huduma ya
upasuaji kwa watoto ambao baadhi yao wazazi wao hawana uwezo wa
kuwapeleka nchini India.
“Pia
nimefarijika kukuta kiwanda chako kipo hai na kinafanya kazi nzuri ya
kusalisha magodoro bora. Nakupongeza kwa kutekeleza wito wetu wa kutoa
kipaumbele cha ajira kwa kuajiri Watanzania 147 kati ya watumishi 150
walioajiriwa kiwandani hapa,” alisema.
Bw.
Gulamali alisema anatarajia kuwekeza katika ujenzi wa mradi wa kiwanda
cha kusindika mafuta ya alizeti kitakachogharimu sh. bilioni nne hivyo
kitaongeza fursa ya ajira kwa Watanzania.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, OKTOBA 02, 2016
0 Comments
on