Wakati polisi ikizuia mkutano mkuu maalumu wa CUF uliopangwa kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad mjini Tanga jana, mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba alifanya usafi soko la Buguruni, huku akilindwa na jeshi hilo. 
Lipumba alifanya kazi hiyo akitekeleza agizo la Rais John Magufuli la kufanya usafi Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi. Msemaji wa CUF, Abdul Kambaya alisema haoni kama ni jambo la ajabu kwa Lipumba kufanya usafi wakati akilindwa.

“Sioni mantiki ya swali hilo, suala la kulindwa Lipumba siyo wa kwanza,” alisema 
Mapema jana, polisi mjini Tanga ilizuia mkutano uliopangwa kuhudhuriwa na Maalim Seif ambao ulipaswa kuwajadili madiwani 12 waliopigana wiki iliyopita katika ofisi za chama hicho wilayani humo, baada ya kugawanyika kuhusu uamuzi wa wenzao waliohudhuria baraza la madiwani wa jiji hilo Oktoba 12.

Taarifa ya jeshi hilo ilidai kuzuiwa kwa mkutano huo ni kutokana na tisho la uvunjifu wa amani na kuwapo kwa makundi mawili yanayozozana. Mkutano huo ulipangwa kufanyika katika Hoteli ya Mkonge mjini hapa.

Pia, taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tanga, Idd Abdallah ilisema ukumbi ambao mkutano huo ungefanyika ni mdogo kutokana na wingi wa wanachama.

 “Ukumbi uliopangwa kufanyika kwa mkutano huo ni mdogo na ikumbukwe kuwa wiki iliyopita mkutano wa chama hicho ngazi ya wilaya ulivunjika kutokana na vurugu,” alisema
Akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa CUF wa wilaya hiyo, Rashid Jumbe alisema hata kama jeshi hilo limezuia mkutano huo, lengo la chama kuwajadili madiwani hao liko palepale. 
Alisema kamati ya utendaji imependekeza madiwani saba kati ya 12 wafukuzwe uanachama kutokana na kukiuka msimamo wa chama na watano watabaki chini ya uchunguzi.

“Katika fagio hili mbunge (Mussa Mbaruku) pia yumo kwani naye alishiriki kikamilifu pamoja na naibu meya (Mohamed Aniu), kwa sasa tunafanya utaratibu na jeshi la polisi kutekeleza masharti na vigezo wanavyotaka ili kuufanya mkutano huo tena,” alisema.


==