Kampuni ya Kikorea inayojishughulisha na utengenezaji wa bidhaa za umeme, Samsung imesitisha utengenezaji wa toleo lake jipya a simu za Samsung Galaxy Note 7 kutokana na milipuko ya betri za simu hizo.
Hapo awali kampuni ya Samsung iliwataka wateja wake kurudisha simu hizo na kubadilishiwa na toleo jipya ambalo lilionekana kutokuwa na mapungufu hayo, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida matoleo hayo mapya pia yameripotiwa kushika moto.
Samsung imeamua kuwashauri watumiaji wa simu hizo kuzizima na kuacha kuzitumia huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufanyika.
Zaidi ya matukio 36 ya kushika moto kwa simu hizo yameripotiwa duniani kote na kuyafanya makampuni makubwa ya mitandao ya simu ya nchini Marekani kama AT&T kutangaza kusitisha uuzaji wa simu hizo huku T-Mobile ya Ujerumani nayo ikitangaza kufanya hivyo.
Mpaka leo asubuhi mauzo katika soko la hisa nchini Korea Kusini yanaonyesha kushuka kwa asilimia 5, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kutokea katika mwaka huu kwa kampuni ya Samsung.


0 Comments
on