Serikali
imeiagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kusitisha mara
moja makato ya fedha yaliyokuwa yakifanywa kwenye malipo ya pensheni ya
mstaafu Ernest Lameck, katika Chuo cha Ualimu cha Tukuyu kilichopo
wilayani Rungwe.
Agizo
la kusitishwa kwa makato hayo limetolewa baada ya kubainika kuwa deni
hilo ni hewa kwa kuwa mtumishi huyo mstaafu hakuwahi kusoma katika chuo
cha Elimu ya Juu.
Amesema Bodi ya Mikopo imekuwa ikitoa mikopo na kwamba kinachofanywa na taasisi hiyo ya Serikali ni wizi.
Waziri
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako, ametoa agizo hilo jana alipofanya ziara katika Chuo cha
Ualimu Tukuyu na kuelezwa juu ya uwepo wa mstaafu huyo ambaye amekuwa
akikatwa fedha wakati si mnufaika wa mkopo.
Mkuu
wa chuo hicho, Ubaya Salumu, amemweleza Waziri kuwa Lameck aliyekuwa
mtumishi chuoni hapo alianza kukatwa fedha kwenye pensheni yake na
alipofuatilia alibaini kuwa makato yamekuwa yakifanywa na Bodi ya
Mikopo.
Amesema
jambo la kushangaza ni kuwa kabla na wakati wa utumishi wake, Lameck
hakuwahi kusoma elimu ya juu ambayo angeweza kuomba mkopo kutoka katika
bodi hiyo.
Lameck
amebainisha kuwa baada ya kufuatilia alibaini kuwa Bodi ya Mikopo
inamdai Sh milioni tisa na ni kwa muda mrefu amejaribu kufuatilia jambo
hilo pasipo mafanikio.
Kutokana
na hali hiyo, Profesa Ndalichako mbali na kuiagiza bodi kusitisha
makato hayo mara moja, pia aliagiza fedha zote alizokatwa mtumishi huyo
zirejeshwe ili anufaike na stahili zake.
“Haiwezekani
mtu haukukopeshwa halafu waanze kumkata. Hili nataka lifanyike haraka
na si tu kusitisha makato, bali lazima Bodi wakulipe fedha zako zote
walizokukata,” alisisitiza.
0 Comments
on