Serikali
imewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Mafia na Watanzania wote kuwa
Kisiwa cha Shungi Mbili kilichopo wilayani humo mkoani Pwani,
hakijakodishwa wala kuuzwa kwa mtu yeyote kama inavyodaiwa na baadhi.
Badala
yake, serikali imeingia mkataba na mwekezaji kwa ajili ya kufanya
biashara ya hoteli ya kitalii ya hadhi ya nyota tano katika kisiwa hicho
kwa kipindi cha miaka 20, uwekezaji ambao una manufaa zaidi kwa
wananchi na serikali kwa ujumla.
Akizungumza
wakati wa hafla ya uzinduzi wa hoteli hiyo iliyopewa jina la Thanda,
Meneja Mkuu wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini, Dk Milali
Machumu alisema mwekezaji huyo ameingia mkataba huo na serikali kufanya
biashara hiyo ikiwa ni sehemu ya kukiendeleza Kisiwa cha Shungi Mbili
ambacho kilikuwa hakikaliwi na watu.
“Mimi
niwahakikishie tu Watanzania kwamba serikali iliyoko madarakani chini
ya Rais John Pombe Magufuli ipo makini na hizo tetesi za kuuzwa kwa
kisiwa hiki mzipuuze, kwani kama mnavyoona pamejengwa hoteli ya kitalii
kwa makubaliano na serikali na sio kuuzwa wala kukodishwa,” alisema Dk Machumu.
Alisema
kufunguliwa kwa hoteli hiyo kutainufaisha serikali kwa kupata mapato
kupitia kodi na kutengeneza ajira kwa wakazi wa Mafia pamoja na
kuchochea maendeleo na pia wamezingatia sheria ya utunzani wa mazingira
ya baharini.
Mkuu
wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Nunduma alisema kufunguliwa kwa hoteli hiyo
kumetoa fursa nzuri ya ajira kwa wakazi wake na pia kutachochea kasi ya
maendeleo kwa wilaya hiyo.
Mkurugenzi
Mkuu wa hoteli hiyo, Pierre Delvaux aliishukuru serikali kupitia kwa
Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Dk Machumu kwa kuwezesha
uwekezaji huo, ambao machakato wake ulianza miaka 10 iliyopita.
Delvaux
alisema hoteli hiyo ina vyumba vitano vya kulala, bwawa la kuogelea,
maeneo ya michezo kama tenisi pamoja na vitu vyote vya kufurahisha na
gharama yake ni Dola za Marekani 10,000 (sawa na zaidi ya milioni 20)
kwa usiku mmoja.
Pia
alisema wamezingatia manufaa kwa wakazi wa Mafia na hivyo kwa upande wa
ajira asilimia 65 itakuwa ni kwa wakazi wa kisiwa hicho.
“Leo tumeizindua rasmi hoteli hii, lakini itaanza kufanya kazi katikati ya Novemba mwaka huu,” alisema Delvaux.
Kisiwa
cha Shungi Mbili ambacho ni sehemu ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani ni
miongoni mwa visiwa 15 ambavyo ni maeneo tegefu vilivyopo katika Bahari
ya Hindi na hairuhusiwa kufanya shughuli yoyote ya uvuaji wa samaki.
0 Comments
on