WAZIRI
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema atalifumua
na kuliunda upya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kwamba wameshaanza
kutafuta vijana 136 watakaoajiriwa katika shirika hilo kwa lengo la
kudhibiti bidhaa, zinazoingizwa nchini chini ya viwango.
Aidha,
wataweka kitengo maalumu kwa vijana hao, watakaokuwa na uwezo wa
kuchunguza mipaka ya nchi, kunusanusa katika bandari bubu, kukamata,
kuwasiliana na Polisi na kusimama mahakamani kutoa ushahidi.
Mwijage
aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wa utoaji wa tuzo kwa
washiriki wa Programu ya Kaizen iliyo chini ya Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Alisema
lengo la kuiunda upya TBS ni kuhakikisha kwamba kazi zinafanyika
ipasavyo ili kulinda viwanda vya ndani, vinavyozalisha bidhaa
mbalimbali.
“Tutahakikisha
kwamba hakuna bidhaa zitakazoingia bandarini bila ya kuwa na viwango
vinavyotakiwa. Lengo ni kuwalinda walaji na viwanda vyetu, kwa nini
tuagize vitu nje wakati viwanda vyetu vinazalisha bidhaa,’’ alisema Mwijage.
Hatua
yake hiyo imekuja siku chache, baada ya makontena 100 kutoroshwa katika
bandari kavu za Dar es Salaam bila ya kukaguliwa na hivyo kuikosesha
mapato serikali na pia kuwa na hatari ya kuingiza bidhaa zilizo chini ya
kiwango.
Akizungumza
utekelezaji wa agizo la Mwijage na hadi Jumanne wiki hii kwa
waliotorosha makontena hayo kujisalimisha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS,
Dk Egid Mubofu alisema jana kuwa waziri ameongeza siku za utekelezaji
wa agizo lake la kuwataka wafanyabiashara walioingiza maontena 100
bandarini bila kukaguliwa na TBS, watoe taarifa.
Dk
Mubofu alisema baada ya agizo la awali, lililokuwa linamalizika Jumanne
Oktoba 18, waziri aliongeza hadi leo ndipo hatua stahiki zichukuliwe.
Hata
hivyo, alisema mwitikio umekuwa mkubwa na baada ya majumuisho ya leo,
atakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa taarifa kuhusu suala hilo.
Septemba
13, Mwijage alitoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena
100 bandarini bila kukaguliwa na TBS, wakatoe taarifa katika shirika
hilo.
Mwijage
alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa
siku hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia
15.
Akizungumzia
Programu ya Kaizen, Waziri Mwijage alisema jambo linalotakiwa kwa sasa
ni kuhakikisha kwamba viwanda vingi, vinakuwa na mfumo huo wa Kaizen,
kwani utasaidia kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango vya hali ya juu.
Alisisitiza
lazima wafanyabiashara waboreshe bidhaa zao na kwamba wasitengeneze
bidhaa kumtosheleza mteja bali kumridhisha mteja.
“Hatutaki
kuingiziwa bidhaa ‘midabwada’ wala mataputapu, tunachotaka ni bidhaa
zenye viwango vinavyotakiwa na tunataka wazalishaji wetu mzalishe bidhaa
zenye viwango na viwango vya kimataifa kwa ajili ya kuuza nje ya
nchi,’’ alifafanua.
Hata
hivyo, alisema sababu ya viwanda kufa ni baada ya kufunguliwa milango
ya bidhaa kutoka nje kuingia nchini, ambazo hazikukidhi viwango na
kwamba wafanyabiashara kutoka nje walikuwa wanashindana na
wafanyabiashara waliopo, ambao waliwekeza fedha nyingi katika miradi
yao.
Kwa
mujibu wa Mwijage, mpango huo wa Kaizen umefanywa katika mikoa mitatu
ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma ambapo umesaidia kuongeza tija
katika uzalishaji na kupunguza upotevu wa malighafi.
Aidha,
aliwataka Watanzania kupenda vitu vya nyumbani kwani wanahakikishiwa
ubora na endapo vitakuwa na tatizo ni rahisi kuwabana wafanyabiashara wa
ndani kuliko wa nje.
Kwa
upande wake, Mwakilishi wa JICA nchini, Toshio Nagase alisema mpango
huo umesaidia kufundisha wakufunzi kwenye kampuni na viwanda zaidi ya 50
vilivyopo nchini.
Nagase
alisema Kaizen imeleta matokeo kwa vitendo kwenye maeneo ya biashara
kwa njia ya kusafisha eneo, kupunguza malighafi, kuhakikisha ubora wa
bidhaa na kubadilisha tabia au motisha kwa wafanyakazi.
‘’Tunaamini
kwamba Kaizen ni jambo muhimu katika kutengeneza viwanda vyenye
ushindani kibiashara na kufanikisha lengo la kukuza viwanda kuelekea
mwaka 2025,’’ alisema.
Alisisitiza
kuwa mradi huo wa miaka mitatu, ulianza mwaka 2013 na kwamba ulianza
Japan na nchi za Afrika unatekelezwa katika nchi za Ethiopia, Tunisia,
Misri, Ghana, Zambia na Tanzania.
0 Comments
on