Licha
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutotekeleza adhabu ya
kifo kwa zaidi ya miaka 20. Imeendelea kusisitizwa kuifuta sheria ya
adhabu ya kifo kwa watuhumiwa wa makosa ya mauaji kwa kuwa haisaidii
kupunguza makosa hayo na kwamba iangalie chanzo cha tatizo hilo kwa
lengo la kufanyia marekebisho.
Ushauri huo umetolewa jana
na wadau mbalimbali wa haki za binadamu katika kongamano la kuijadili
adhabu ya kifo nchini, lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN).
Wadau hao walisema
kuwa, falsafa ya ukuaji wa adhabu huzingatia vigezo viwili ambavyo ni
kutoa funzo kwa jamii pamoja ma kumrekebisha mkosaji. Wadau hao waliitumia
hoja hiyo kuisisitiza serikali kufuta adhabu ya kifo kwa kuwa endapo
mtuhumiwa akiuawa hatopata fundisho na pia kifo chake kinatafsiriwa sawa
na kosa hilo kujirudia.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Hellen Kijo-Bisimba alisema
kituo hicho hakitaacha kuishauri serikali kuifuta adhabu hiyo kwa kuwa
haisaidii kutokomeza matukio ya mauaji na pia huenda ikaathiri watu
wasio na hatia.
“Inabidi
serikali iangalie chimbuko la matukio ya mauaji ili litokomezwe na si
kuhukumu watu kwa adhabu ya kifo, hatumaanishi wasihukumiwe bali
watafutiwe adhabu nyingine kwa kuwa tangu kuanza kutumika adhabu hii
matendo ya mauaji hayajapungua,” alisema.
Aliongeza kuwa ”
Kumuua mtu si suluhisho bali kosa hilo linazidi kufanyika na si sahihi.
LHRC tunaendelea kuipinga adhabu hii sababu haisaidii kupunguza
mauaji,”
Bisimba alidai
kuwa, asilimia kubwa ya wanaohukumiwa adhabu ya kifo ni watu wasio na
kipato na kwamba hali hii huonyesha adhabu hiyo hutekelezwa kitabaka
zaidi.
Mwakilishi wa UN, Roeland Van de Geev alisema
kuwa shirika hilo halitailazimisha serikali kuifuta sheria hiyo bali
litawezesha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) yanayohusika na haki
za binadamu nchini kuishauri serikali kufuta adhabu hiyo.
“Nchi
zaidi ya 140 duniani zimefuta adhabu hiyo, na hakuna matukio ya kutisha
ya mauaji katika nchi husika, mfano Marekani inatekeleza adhabu ya kifo
lakini matukio ya mauaji bado yanaendelea. Hii inamaanisha kwamba
suluhu pekee ni kutibu au kuzuia vyanzo vya matukio hayo,” alisema.
Alishauri kuwa “Adhabu
hii hafai kutekelezwa sababu inaondoa utu wa mtu. Tanzania pamoja na
nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki zifute sheria hiyo.”
Bahame Tom Nyanduga kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora alisema
adhabu hiyo haistahili kuendelea kutekelezwa nchini kutokana kwamba
ilianzishwa na wakoloni kwa lengo la kulinda utawala wao.
“Haki
ya binadamu ya kuishi ndiyo msingi wa haki nyingine, katiba ya 1977
inatambua haki ya kuishi. Mahakama haiwezi futa adhabu hii bali serikali
ndiyo yenye wajibu wa kuifuta sheria hiyo hivyo ni vyema ikafanya
hivyo,” alisema.
Alisema
ingawa serikali haijatekeleza adhabu hiyo kwa zaidi ya miaka 20 lakini
inawajibu wa kuifuta sababu watu wanazidi kuhukumiwa.
“Nchi
zaidi ya 20 Afrika zimefuta adhabu hii na hatusikii kama kuna kukithiri
kwa matukio ya mauaji.Ni vigumu kuhusisha adhabu ya kifo kama suluhisho
pekee la kutokomeza mauaji,” alisema.
Sheikh Ally Hemko kutoka Baraza Kuu la Waisilamu Tanzania (Bakwata) alishauri jamii kuepukana na vitendo vya mauaji kwa kuwa dini hairuhusu.
“Dini
yetu hufundisha kuwa mtu anayeua nae aue ingawa pia inasisitiza kuua ni
dhambi hivyo ili kuondokana na utata huo, jamii inawajibu wa kuacha vitendo hivyo sababu hata kama sheria hiyo ikifutwa watu wasio wema watazidi kuua,” alisema.
0 Comments
on