Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Angella Kairuki amesema atahakikisha anawachukulia hatua watendaji
wote, walioshiriki katika udanganyifu wa kuingiza kaya zisizostahili
katika Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaosimamiwa na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Aidha,
aliiagiza Tasaf kuhakikisha inafuatilia kaya zote ambazo ziliingizwa
katika mpango huo bila kuwa na sifa zinazostahili, kwa kuziorodhesha kwa
majina, wanapoishi na kiasi cha fedha walichopokea ili ripoti hiyo
iwasilishwe kwa Rais John Magufuli.
Kairuki
aliyasema hayo jana wakati akizungumza baada ya kupokea ripoti ya
utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf III) ya Mkoa wa
Dar es Salaam, sambamba na kuzungumza na wananchi katika mitaa ya Kigogo
Kati na Mikoroshoni, Manispaa ya Kinondoni.
“Kaya
ambazo hazistahili hawafanyi peke yao wanashirikiana na watu, kama ni
viongozi katika ngazi za mitaa na kata mitaa tunataka majina, na katika
kila jina tujue nani alishiriki kumuingiza nani alikuwa akimchukulia na
kama yupo mtumishi wetu wa umma tujue ni nani na hatua gani za kinidhamu
zimechukuliwa.”
“...Msije mkashangaa nikaja kuelekeza polisi kukamata hawa na hawa kwa sababu hizi hela ni lazima zirudi,” alisema Kairuki.
Alisema
ameshapokea taarifa za mikoa mbalimbali, lakini Dar es Salaam na wilaya
zake bado na mwisho ilikuwa ni Oktoba 6, mwaka huu, lakini aliwaongeza
wiki moja ambayo tayari imeisha na orodha hiyo inatakiwa ipelekwe kwa
Rais Magufuli.
Kairuki
aliongeza kuwa pamoja na mkoa kusema umeondoa kaya 789 ambazo hazina
sifa, lakini kuna kaya 5,457 ambazo zinapaswa kuondolewa katika mpango
huo kwa kuwa hazina sifa za kupokea ruzuku hiyo.
“...baada
ya kuelekeza uhakiki wa nyumba kwa nyumba, sisi kwa taarifa tulizonazo
tutaondoa kaya 5,457. Sasa ujiulize nyinyi ndio mlikuwa katika zoezi na
mkapata idadi hiyo, hapa inaonesha kuna kitu hakipo sawa,” alisema.
Alisema
katika kaya hizo zitakazoondolewa, 1,867 hazina vigezo vya umasikini,
563 zipo kwenye orodha lakini zilikuwa hazijitokezi kuchukua ruzuku na
hazijulikani zilipo na kaya nyingine 2,114 hazikupatikana wala
kujulikana zilipo wakati wa ukaguzi.
Alisema
kaya hizi ni nyingi na hasa ikizingatiwa asilimia 76 hazijaingizwa
katika mpango huo, hivyo kaya hizo ambazo ziliandikishwa zinapaswa
kwenda kukaguliwa ili ziweze kuingizwa katika mpango huo ili katika
awamu ya nane ya uhawilishaji fedha waweze kupata.
Kairuki alisema kiasi kikubwa cha fedha kimepotea, ambacho kingeweza kuwasaidia watu wanaostahili kuwa katika mpango huo.
Alisema
wilaya za Kinondoni na Temeke zimeshapokea malipo ya awamu saba ambayo
ni Sh bilioni 6.7. Alisema hadi sasa kuna kaya 32,456 zilizoondolewa
kwenye mpango huo.
Kwa wastani kaya moja hulipwa kati ya Sh 20,000 hadi 60,000 kwa kutegemea idadi ya watu katika kaya.
Akizungumza
katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi ambaye pia ni
Kaimu Mkuu wa Mkoa alisema mpango huo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa,
lakini kuna watu wanaoharibu taswira ya Tasaf.
Alisema kuna fedha nyingi ambazo zinaishia kwenye mikono ya wajanja na haziwafikii walengwa wa mpango huo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga alisema
mpango huo umeandaliwa kitaalamu na utaendelea kuwa endelevu na kwamba
mradi huo unategemea zaidi serikali na wafadhili, lakini hadi sasa kiasi
kikubwa kimekuwa kikitoka kwa wafadhili.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala bora
Mh. Angela Kairukia akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni,akiendelea na ziara katika Mkoa wa Dar es salaam kukagua
maendeleo ya mradi wa kusaidia kaya masikini TASAF
0 Comments
on