WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Bw. Bakari Mohammed kuhakikisha
hospitali ya wilaya hiyo inakusanya mapato kwa kutumia mfumo wa
kielektroniki.
Ametoa
agizo hilo jana Jumapili, Oktoba 16, 2016 wakati alipotembelea
hospitali ya wilaya ya Nachingwea akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya
siku tatu mkoani Lindi.
Waziri
Mkuu amesema Serikali ilishaagiza taasisi zote za umma kutumia mfumo wa
kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kudhibiti mianya
ya upotevu wa fedha za umma.
Amesema
taasisi ambazo tayari ziameanza kutumia mfuko huo katika ukusanyaji wa
mapato zimeweza kuongeza kiwango cha makusanyo kutoka sh. 300,000 hadi
milioni nne kwa siku.
Pia
aliwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuwahamasisha wananchi
kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao utawawezesha kupata
huduma ya matibabu bure katika kipindi cha mwaka mzima.
Akizungumzia
kuhusu matibabu kwa wazee, Waziri Mkuu amemuagiza Bw. Mohammed
kuhakikisha anafungua dirisha la kuwahudumia wazee ili kuwarahisishia
upatikanaji wa huduma wanapofika hospitalini hapo.
“Mkurugenzi
hakikisha watendaji wako wa kata na vijiji wamebaini wazee wote katika
maeneo yao na kuwatengenezea vitambulisho vitakavyowawezesha kupatibiwa
bure,” amesema.
Naye
Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dk. Samwel Laizer amesema muamko mdogo wa
jamii kujiunga na CHF ni moja kati ya changamoto zinazowakabili katika
utoaji wa huduma za afya.
Dk. Laizer amasema kati ya kaya 30,000 zilizoko wilayani Nachingwea ni kaya 7,133 tu ndizo zilizojiunga na mfuko wa CHF.
Awali
Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa wilaya hiyo kwenye ukumbi wa
Chuo Cha Walimu na kuwataka wabadilike ili waweze kuwatumikia wananchi
kwa uadilifu bila ya kujali itikadi zao za kidini na kisiasa.
Amesema
Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayeshindwa kutekeleza wajibu
wake wa kuwatumikia wananchi. “Serikali haitaridhika kuona wananchi
wakizagaa kwenye ofisi za halmashauri hiyo bila ya kusikilizwa,”
amesema.
0 Comments
on