MAHAKAMA ya Wilaya ya Kongwa imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Lazaro Madeha (56) kwa kupatikana na hatia ya kujaribu kumbaka mtoto wake wa kambo wa miaka tisa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Marry Senapee alisema Mahakama yake ilijiridhisha na ushahidi uliotolewa. Alisema ndiyo sababu imetoa adhabu hiyo iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo za ukatili kwa watoto wadogo.
Awali, Mwendesha mashtaka wa Polisi, Mkaguzi msaidizi, Kandoro Babile alidai mtuhumiwa alitenda kosa hilo Juni 26 mwaka huu katika Kijiji cha Mkoka wilayani Kongwa. Alidai mtuhumiwa alimkamata mtoto huyo na kumuingiza chumbani kwake.
“Baada ya mtuhumiwa huyo kumuingiza mtoto huyo wa kambo chumbani kwake alimvua nguo zote huku naye akiwa mtupu na kutaka kumbaka. Mtuhumiwa Madeha alikuwa anataka kumbaka mtoto huyo baada ya mama wa mtoto kwenda kisimani kuchota maji na aliporudi alimkuta mtuhumiwa akiwa mtupu kitandani yeye pamoja na mtoto akitaka kumbaka. Mama huyo alipiga kelele na majirani walifika na kumkamata,”alisema.
Mwendesha mashitaka aliiomba Mahakama kumpa adhabu kali mtuhumiwa iwe fundisho kwa wengine weye tabia kama hizo.